Michezo

Hatimaye Oktay ajiuzulu,Gor kutangaza kaimu kocha mpya Alhamisi

August 7th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CECIL ODONGO

UONGOZI wa Mabingwa mara 18 wa Ligi Kuu(KPL) Gor Mahia, unatarajiwa kutangaza kaimu kocha mpya kesho baada ya Hassan Oktay kujiuzulu Jumanne.

Oktay, raia wa Uturuki, aliomba klabu hiyo kutafuta huduma za kocha mwingine baada ya siku tano alizoomba kutatua masuala ya kifamilia nchini kwao kukamilika.

Mkufunzi huyo aliteuliwa Desemba 2018 kuinoa Gor Mahia baada ya Dylan Kerr ambaye pia aliongoza timu hiyo kwa msimu mmoja kujiuzulu.

“Nimejiuzulu kama kocha Mkuu wa Gor Mahia. Jinsi mnavyofahamu nimelazimika kuafikia uamuzi huo kutokana na changamoto za kibinafsi ninazopitia hapa nyumbani,” akasema Oktay kwenye taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa klabu.

Akaongeza: “Ningependa kushukuru klabu pamoja na mashabiki kwa kunipa nafasi ya kuongoza klabu. Ninawatakia kila la kheri kwenye mechi zenu.”

Uongozi wa K’Ogalo ulijibu kwa kusema wamekubali kujiuzulu kwa Oktay na kumshukuru kwa huduma alizowapa.

“Klabu imekubali uamuzi wa Oktay kukatiza rasmi kandarasi yake na tunamshukuru kwa huduma alizotoa. Klabu inamwombea ushindi kwenye changamoto anazokumbana nazo,” ikathibitisha Gor Mahia kwenye mtandao wao.

Uwezo wa kufika mbali

Kabla ya kuondoka nchini kutatua masuala ya kifamilia, Oktay alisema kwamba timu hiyo inaweza kufika mbali bila huduma zake, matamshi yaliyofasiriwa kwamba huenda ameagana na Gor Mahia na kwa kweli yalitimia jana

Awali Mwenyekiti wa K’Ogalo, Ambrose Rachier alieleza Taifa Leo kwamba Oktay hakuwa amewasiliana naye tangu asafiri siku tano zilizopita hata baada ya siku alizopewa za kutatua masuala ya kifamilia kukamilika na akasema hawana budi ila kutafuta kocha mpya.

“Kocha wetu hajawasiliana nasi tangu asafiri hata baada ya siku nane tulizompa kukamilika. Alituahidi kwamba angetufahamisha kama angerejea au la baada ya muda huo lakini hajafanya hivyo. Tutaandaa mkutano na kutangaza kocha mpya kesho kabla ya mechi ya Jumapili,” akasema Rachier.