Michezo

Henry, Pochettino, Koeman na Xavi kati ya makocha wanaohusishwa na mikoba ya Barcelona

August 16th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

NGULI wa soka wa Arsenal na timu ya taifa ya Ufaransa, Thierry Henry, 42, ni miongoni mwa wakufunzi wanaohusishwa na uwezekano mkubwa wa kupokezwa mikoba ya ukocha kambini mwa Barcelona.

Barcelona wanatazamiwa kumtimua kocha Quique Setien baada ya miamba hao wa Uhispania kudhalilishwa na Bayern Munich kwa kichapo cha 8-2 kwenye robo-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na hatimaye kukamilisha kampeni zao za msimu huu bila taji lolote.

Kwa mujibu wa gazeti la Mundo Deportivo nchini Uhispania, Henry ambaye kwa sasa ni kocha wa kiungo wa Harambee Stars Victor Wanyama kambini mwa Montreal Impact nchini Canada, yuko pazuri zaidi kuwapiku wakufunzi wengine watakaowania fursa ya kurithi mikoba ambayo Setien atapokonywa ugani Camp Nou.

Henry aliwahi kuvalia jezi za Barcelona kwa kipindi cha misimu mitatu akiwa mchezaji kabla ya kuangika daluga na kujitosa katika ulingo wa ukocha. Hata hivyo, hakufanya vyema katika kambi ya AS Monaco, Ufaransa waliompa fursa ya ukufunzi.

Mbali na Henry, wakufunzi wengine wanaohusishwa na mikoba ya Barcelona ni kocha wa zamani wa Tottenham Hotspur Mauricio Pochettino na aliyekuwa mkufunzi wa Everton, Ronald Koeman.

Koeman, ambaye amekuwa kocha wa timu ya taifa ya Uholanzi tangu 2018, aliwahi kuvalia jezi za Barcelona kwa miaka sita akiwa mchezaji kati ya 1989-1995.

Kwa upande wake, Pochettino ambaye ni mzawa wa Argentina na rafiki wa karibu wa Bartomeu, hajawahi kupata klabu ya kunoa tangu atimuliwe na Tottenham mnamo Novemba 2019.

Mwingine ni kiungo wa zamani wa Barcelona, Xavi Hernandez, 40, ambaye kwa sasa anadhibiti mikoba ya kikosi cha Al-Sadd nchini Qatar.