• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 4:33 PM
Higuain mjanja wa kupiga chenga, hela zake zaweza kukausha bahari

Higuain mjanja wa kupiga chenga, hela zake zaweza kukausha bahari

Na CHRIS ADUNGO

GONZALO Higuain, 31, ni mshambuliaji matata anayeipigia soka timu ya taifa ya Argentina na klabu ya AC Milan kwa mkopo wa miaka miwili kutoka kwa wafalme wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A), Juventus.

Hadi alipotua Milan, mgongo wa Higuain kimshahara ulikuwa ukisomwa kwa karibu na Miralem Pjanic, Blaise Matuidi na Emre Can, viungo ghali zaidi wanaopokezwa mshahara wa Sh720 milioni kwa mwaka na Juventus.

Alikuwa ndiye mchezaji wa tatu kudumishwa kwa mshahara wa juu kabisa katika Ligi Kuu ya Serie A baada ya Cristiano Ronaldo na Daniele De Rossi wa Juventus na AS Roma mtawalia.

Higuain kwa sasa anatarajiwa kutua ugani Stamford Bridge kuvalia jezi za Chelsea katika uhamisho utakaomshuhudia mvamizi Alvaro Morata akichukua nafasi yake kambini mwa Milan.

UTAJIRI: Thamani ya mali ya Higuain inakadiriwa kufikia Sh6 bilioni na kiini kikubwa cha utajiri wake ni mshahara wa Sh16 milioni aliokuwa akipokezwa kwa wiki na Real Madrid kabla ya Napoli kuzinyakua huduma zake kwa ahadi ya Sh74 milioni kila mwezi.

Ilikuwa hadi mwanzoni mwa 2015 ambapo Higuain alitia saini kandarasi mpya na Napoli katika maelewano yaliyomshuhudia akidumishwa kwa Sh28 milioni kila wiki kabla ya huduma zake kutwaliwa na Juventus.

Kwa kipindi hicho, thamani ya Higuain ilivumishwa sana kiasi kwamba kikosi chochote ambacho kingethubutu kuyahemea maarifa yake kingelazimika kuweka mezani zaidi ya Sh8 bilioni ili kuwashawishi Napoli kumwachilia. Mbali na mshahara mkubwa ambao kwa sasa Milan wanampa, Higuain hujirinia fedha za ziada kutokana na maru- purupu na bonasi za kushinda mechi katika ngazi za klabu au timu ya taifa.

Isitoshe, ni balozi wa kutangaza bidhaa za kampuni za Nike na Electronic Arts (EA Sports) ambayo humpokeza hadi Sh59 milioni kila mwezi. Higuain bado ana mkataba wa miaka miwili na Nike ambayo humpokeza kitita cha Sh202 milioni kwa mwaka.

Aidha, yupo katika mkataba wa Sh170 milioni kwa mwaka na kampuni ya KFC ya Arabia ambayo hutengeneza vinywaji na vitafunio. Kwa ufupi, Higuain hujipatia takriban Sh1.8 bilioni kwa mwaka, pesa ambazo huenda ikamchukua Mkenya wa kawaida anayepata mshahara wa Sh20,000 kwa mwezi zaidi ya miaka 7,500 kujikusanyia.

MAKASRI: Higuain ana maskani yenye thamani ya Sh700 milioni jijini Turin, Italia. Anamiliki majengo mengine ya kifahari katika majiji ya Naples, Roma na Madrid huku kasri alilowajengea wazazi wake mnamo 2010 jijini Buenos Aires, Argentina likimgharimu Sh405 milioni.

MAGARI: Maegeshoni pa Higuain hupatikana magari ya kifahari aina ya Audi Q7 lililomgharimu Sh24 milioni, Ferrari 458 la Sh17 milioni na Range Rover Sport lililomgharimu Sh26 milioni mwanzoni mwa mwaka huu. Haya ni magari matatu tu miongoni mwa mengi ya haiba kubwa anayoyaendesha nyota huyo anayejivunia maguu ya dhahabu.

MAPENZI: Tetesi kwamba Higuain alikuwa akitoka kimapenzi na mwanahabari mzawa wa Uhispania, Daniela Saurwald mnamo 2013 zilimfanya apoteze kichuna mwigizaji wa Argentina, Soledad Fandino. Ingawa hivyo, ilimchukuwa Higuain miezi mitatu pekee kujinasia penzi la mrembo Lucia Fabian.

You can share this post!

Torreira mwili wa chuma katika ngome ya Arsenal

Kichapo kutoka kwa Man-City hakina uwezo wa kuzima ari ya...

adminleo