• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 4:43 PM
Hofu PSG baada ya Mbappe na Cavani kupata majeraha

Hofu PSG baada ya Mbappe na Cavani kupata majeraha

Na MASHIRIKA

PARIS, UFARANSA

KOCHA Thomas Tuchel wa Paris Saint-Germain (PSG) amekiri kwamba kuumia kwa washambuliaji Kylian Mbappe na Edinson Cavani ni pigo kubwa kwa kampeni za kikosi chake.

Nyota hao wawili walipata majeraha yanayotarajiwa kuwaweka mkekani kwa kipindi cha wiki kadhaa walipokuwa wakiwachezea waajiri wao dhidi ya Toulouse mwishoni mwa wiki iliyopita.

Cavani ambaye ni mzaliwa wa Uruguay alilazimika kuondoka uwanjani kunako dakika ya 14 huku Mbappe akitolewa katika kipindi cha pili baada ya kupata jeraha la paja.

Ingawa hivyo, PSG ambao wanajivunia ukiritimba mkubwa katika soka ya Ufaransa walisajili ushindi mnono wa 4-0 katika mchuano huo uliochezewa mbele ya mashabiki wao wa nyumbani uwanjani Parc des Princes.

Eric Maxim Choupo-Moting wa Cameroon aliwajibishwa katika nafasi ya Cavani. Ndiye aliyewafungulia PSG ukurasa wa mabao kabla ya Mathieu Goncalves kujifunga na kuwapa wenyeji wao bao la pili bila jasho.

Japo Angel Di Maria alipoteza mkwaju wa penalti, bao la pili kutoka kwa Choupo-Moting na jingine lililofungwa na Marquinhos lilitosha kuwavunia PSG alama tatu muhimu.

PSG bado walikosa huduma za fowadi Neymar Jr katika mchuano huo hasa ikizingatiwa kwamba nyota huyo mzaliwa wa Brazil anahusishwa na uwezekano mkubwa wa kurejea Batcelona au kutua kambini mwa Real Madrid ambao bado wanatafuta kizibo kamili cha Cristiano Ronaldo aliyeyoyomea Juventus mwanzoni mwa msimu uliopita.

Ushindi huo wa PSG uliwakweza hadi nafasi ya tatu jedwalini kwa alama sita sawa na Lyon, Nice na Angers.

Rennes wanaselelea kileleni mwa jedwali kwa alama tisa baada ya kusajili ushindi katika michuano yote mitatu ya ufunguzi wa kampeni za msimu huu.

Iwapo wataagana na Neymar, PSG wamefichua azma ya kumshawishi fowadi Wilfried Zaha wa Crystal Palace kujiunga nao kwa kima cha Sh13 bilioni.

Ujumbe wa PSG tayari umetua jijini London, Uingereza kuanzisha mazungumzo na Palace kwa lengo la kurasimisha uhamisho wa Zaha.

Kwa upande wao, PSG wametaka Barcelona au Real kuweka mezani kiasi cha Sh26 bilioni ili kumsajili Neymar kufikia Septemba 2.

Kiasi cha Sh13 bilioni ambazo Palace waliwataka Arsenal au Everton kuwapa kwa ajili ya Zaha mwishoni mwa msimu uliopita ni bei iliyowakunjisha mikia miamba hao wa soka ya Uingereza.

Zaidi ya kuyahemea maarifa ya Zaha, PSG pia wanawania huduma za Paulo Dybala wa Juventus.

Chini ya kocha Maurizio Sarri, Juventus wanapania sana kuzinadi huduma za Dybala ili fedha zitakazopatikana baada ya kuuzwa kwake ziwawezeshe kujitwalia maarifa ya Christian Eriksen kutoka Tottenham Hotspur.

Zaha alihusishwa na uwezekano mkubwa wa kuingia katika sajili rasmi ya Bayern kabla ya kikosi hicho cha kocha Niko Kovac kujinasia huduma za kiungo Philippe Coutinho wa Brazil kwa mkopo wa mwaka mmoja kutoka Barcelona walipokosa pia kumsajili Leroy Sane wa Manchester City.

Kubwa zaidi katika maazimio ya Bayern limekuwa ni kujaza nafasi zilizoachwa na maveterani Arjen Robben na Franck Ribbery.

Awali, Bayern walikuwa pia wakihusishwa na uwezekano mkubwa wa kujinasia maarifa ya mvamizi Callum Hudson-Odoi kutoka Chelsea baada ya juhudi za kumshawishi Gareth Bale wa Real Madrid kujiunga nao kuambulia pakavu.

You can share this post!

K’Ogalo, Bandari kunyanyuana na wazito wa Afrika

UFISADI: Uhuru azimia marafiki simu

adminleo