Michezo

Hoteli ya Giggs yazama na mamilioni ya pesa za watu

Na MWANDISHI WETU March 27th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MKAHAWA uliokuwa ukimilikiwa na nyota wa zamani wa Manchester United, Ryan Giggs, umezama na mamilioni ya pesa.

Hoteli hiyo ya George’s Dining Room and Bar, ambayo ilifungwa ghafla mwezi jana, Februari 2025, ilikuwa ikidaiwa jumla ya Sh94.7 milioni.

Fedha hizo zilijumuisha pia Sh21.7 milioni za wafanyabiashara waliotoa bidhaa na huduma tofauti Sh12.7 milioni za ushuru na Sh7.4 milioni zilizokuwa mkopo wa benki.

Giggs, 51, alifungua George’s huko Worsley, Greater Manchester mwaka 2014 baada ya kushirikiana kibiashara na Kelvin Gregory na Bernie Taylor ambao ni marafiki waliosoma shule moja jijini Cardiff, Uingereza.

Mwezi uliopita, mkahawa huo ulifungwa ghafla na wafanyakazi wake wote kupigwa kalamu mara moja. Waliarifiwa kupitia arafa za simu kwamba unga wao ulikuwa umemwagika.

Notisi kwenye mlango wa hoteli hiyo wakati huo ilisema kuwa ingesalia kufungwa “kutokana na hali zisizotarajiwa na sababu zisizoepukika.

“Walakini, SMS zilizotumwa baadaye na wakuu wa mkahawa wenyewe kwa wafanyakazi zilisema kuwa mkahawa huo umefungwa kabisa,” Gazeti la Manchester Evening News lilithibitisha.

Jumbe hizo zilisema: “Tanajuta kutangaza kwa moyo mzito kuwa hatuna njia mbadala ila kufunga hoteli ya George’s Dining Room and Bar mara moja kutokana na hali ngumu ya kiuchumi. Tumechukua hatua hii kutokana na kupungua kwa biashara, ongezeko kubwa la gharama za uendeshaji wa biashara na kupanda kwa gharama ya maisha.”

Inasemekana wafanyakazi wote waliambiwa wangelipwa mishahara iliyobaki baada ya muda mfupi, yakiwemo malipo kwa ajili ya notisi ya ghafla ya kukatizwa kwa vibarua vyao pamoja na pesa za kupoteza kazi bila kutarajia kwa wale ambao malipo hayo yanawahusu kwa mujibu wa kandarasi zao. Hayo yote yamesalia kuwa ndoto kwa sasa.

George’s Dining Room and Bar ilipofunguliwa zaidi ya mwongo mmoja uliopita, Giggs alisema ilikuwa ndoto yake ya maisha kumiliki mkahawa wa kifahari sampuli hiyo kwa kuwa ni maono yaliyoanza kumtambuliza pamoja na marafiki zake wa utotoni.

Hafla ya kufunguliwa rasmi kwa hoteli hiyo ilihudhuriwa na wanasoka nguli Bryan Robson, Nicky Butt na Gary Neville waliowahi kucheza pamoja na Giggs kambini mwa Man-United.

Mnamo 2015, mkahawa huo ulipanuliwa kwa kuongezewa orofa ya pili.

Kwa pamoja na mchanganuzi wa masuala ya soka katika Sky Sports, Neville, Giggs pia ni mmiliki wa mikahawa ya Hotel Football at Old Trafford na Stock Exchange Hotel kupitia kampuni ya GG Hospitality Group iliyo na makao makuu jijini Manchester.

Aidha, ana biashara nyingi zinazojihusisha na masuala ya fasheni na uhusiano mwema.

Nyingi za biashara hizo zinaendeshwa sasa na mchumba wake, Zara Charles, 36, aliyejaliwa kimalaika Cora hivi majuzi.