Michezo

Huenda Wanyama akayoyomea China

December 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

NYOTA Victor Mugubi Wanyama huenda akawa Mkenya wa tatu kusakata soka yake ya malipo nchini Uchina baada ya tetesi kuibuka Alhamisi kuwa klabu kadhaa nchini humo zinamezea mate Mkenya huyo.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 28 anasalia mali ya Tottenham Hotspur japo fununu zimekuwa zikiongezeka kuwa timu hiyo kutoka jijini London itamtema katika kipindi kifupi cha uhamisho kitakachofunguliwa Januari 1, 2020.

Akifaulu kuhamia Uchina, Wanyama atafuata nyayo za winga Ayub Timbe na mshambuliaji Michael Olunga waliojiunga na Beijing Renhe na Guizhou Zhicheng mnamo Februari 20 na Januari 24 mwaka 2017, mtawalia.

Olunga sasa ni mali ya Kashiwa Reysol nchini Japan mnamo Agosti 20, 2018 baada ya kukopeshwa kwa klabu ya Girona nchini Uhispania msimu mmoja.

Mbali na Uchina, ripoti nchini Uingereza zinasema kuwa Wanyama anamezewa mate na waajiri wake wa zamani Celtic (Scotland), Hertha Berlin (Ujerumani) na West Ham (Uingereza).

Aidha, Mwenyekiti wa Tottenham Hotspur, Daniel Levy anasemekana yuko tayari kuzuia uhamisho wa Wanyama hadi West Ham mwezi ujao.

Ripoti kutoka jijini London zinasema kuwa kocha mkuu wa West Ham Manuel Pellegrini na mkurugenzi wa soka wa klabu hiyo Mario Husillos wanasemekana kuenzi nahodha huyo wa timu ya taifa ya Kenya.

Wanyama amechezeshwa dakika 122 pekee msimu huu na ameshuhudia akitupwa nyuma ya Eric Dier, Moussa Sissoko, Harry Winks, Tanguy Ndombele na hata Oliver Skipp katika orodha ya wachezaji Tottenham inaweza kuchezesha.

Inasemekana Tottenham haina tatizo kuachilia Wanyama aondoke Januari, lakini Levy atapuuzilia mbali ofa kutoka kwa West Ham kutokana na uhusiano mbovu na bodi ya klabu hiyo, ambayo pia inatoka jijini London.

Wanyama alikaribia kujiunga na Club Brugge ya Ubelgiji katika kipindi kirefu cha uhamisho kilichopita wakati klabu hizi zilikubaliana ada ya Sh1.7 bilioni, lakini mchezaji huyo akajiondoa katika shughuli hiyo dakika ya mwisho.