Ilikuwa vigumu sana kushinda mechi wakati wa Mourinho – Pogba
NA CECIL ODONGO
KIUNGO wa Manchester United Paul Pogba amezidisha uhasama wake na aliyekuwa kocha wake Jose Mourinho, akisema alipata tabu sana kukumbatia mbinu zake za kale za ukufunzi.
Hata hivyo amefunguka na kusema kwamba anayafurahia maisha ugani Old Trafford chini ya kocha mshikilizi Ole Gunnar Solskjaer.
Mchezaji huyo alikuwa na uhasama mkubwa na Mourinho na mara kwa mara alikosa kupangwa katika mechi muhimu kwa kukosa kufuata au kuyatii maagizo ya kocha huyo.
Pogba alikuwa mhimili muhimu wakati wa mechi dhidi ya Tottenham waliyoishinda 1-0 ugani Wembly Jumapili Januari 13. Alitoa pasi ya uhakika kwa mfungaji wa bao hilo la pekee Marcus Rashford katika kipindi cha kwanza kando na kung’aa katika mechi nzima.
Ushindi huo ulifufua matumaini ya United kumaliza ndani ya mduara wa timu nne bora, jambo ambalo lilionekana vigumu kutimia wakati wa Mourinho haswa walipotandikwa 3-1 Liverpool ugani Anfield katika mechi ya mwisho aliyoisimamia mkufunzi huyo.
“Nafurahi sana kusakata soka chini ya kocha mpya kwa sababu anatumia mbinu za ukufunzi zinazosisitizia ufungaji wa mabao badala ya mpira wa kuzuia aliokuwa akipenda sana Mourinho,” akasema Pogba.
Mnyakaji wa Man United David de Gea aliibuka mchezaji bora wakati wa mtanange huo alipozuia au kunyaka mipira mingi kutoka kwa washambulizi Harry Kane na Son.