Ingwe kujaribu kukata kiu ya ushindi ikikutana na Rangers
Na Geoffrey Anene
AFC Leopards itarejea ulingoni kuzichapa dhidi ya Posta Rangers hapo Septemba 15 ikitafuta kufuta vichapo ilivyopokea kutoka kwa Gor Mahia na Wazito katika mechi mbili zilizopita za Ligi Kuu.
Ingwe ilizabwa 2-0 na mahasimu wa tangu jadi Gor mnamo Agosti 25 na kulemewa 2-1 na wanyonge Wazito hapo Agosti 29.
Vijana wa kocha Rodolfo Zapata wameshinda mechi moja pekee katika mashindano yote katika mechi nne zilizopita.
Baada ya kulimwa na viongozi Gor na nambari mbili kutoka mwisho Wazito ligini, Ingwe ilicharaza Kenya Police 4-1 kwenye Soka ya SportPesa Shield, ambayo ni ya kufuzu kuingia Kombe la Afrika la Mashirikisho. Kisha ililizwa 4-2 katika mechi ya kirafiki dhidi ya Simba SC jijini Dar es Salaam nchini Tanzania mnamo Septemba 8.
Leopards inashikilia nafasi ya tatu kwa alama 48 kutokana na mechi 29 katika ligi ya klabu 18. Iko alama 23 nyuma ya mabingwa watarajiwa Gor na alama sita nyuma ya nambari mbili Bandari.
Rangers inafunga 10-bora kwa alama 37 kutokana na idadi sawa ya mechi. Ingwe na Rangers zimekutana mara saba kwenye ligi. Kila mmoja anajivunia ushindi mmoja, huku mechi zingine zote zikimalizika sare.
Ingwe ilikaribisha Rangers kwenye Ligi Kuu kwa kuipepeta 6-2 Aprili 8 mwaka 2012 kabla ya kuchapwa 2-0 Oktoba 14 mwaka 2017. Rangers itaingia mchuano huu na motisha ya kuchabanga Chemelil Sugar 1-0 Septemba 2.
Ezekiel Odera, Alex Orotomal, Brian Marita, Vincent Oburu na Whyvonne Isuza ni baadhi ya nyota Ingwe itatumai wataiongoza kujirejeshea imani ya kushinda. Rangers ya kocha Sammy Omollo, itategemea Dennis Mukaisi, ambaye amepona jeraha la kifundo, na Gearson Likono.
Gor, ambayo itapokea zawadi yake ya kuwa mabingwa mara 17 mwisho wa msimu huu, italimana na wavuta-mkia Thika United hapo Septemba 16.
Ratiba:
Septemba 15, 2018
AFC Leopards na Posta Rangers (4.00pm, Machakos)
Chemelil Sugar na Mathare United (3.00pm, Chemelil)
Nakumatt na Kariobangi Sharks (3.00pm, Camp Toyoyo)
Septemba 16, 2018
Thika United na Gor Mahia (3.00pm, Thika)
Kakamega Homeboyz na Nzoia Sugar (3.00pm, Bukhungu)
Ulinzi Stars na Wazito (2.00pm, Kericho)
Vihiga United na SoNy Sugar (3.00pm, Mumias)
Zoo na Bandari (4.15pm, Kericho)