Ingwe yaahidi kuhifadhi makinda wake wote
Na JOHN ASHIHUNDU
Klabu ya AFC Leopards haitawaruhusu wachezaji wake chipukizi kuondoka klabuni kipindi hiki cha wachezaji kubadilisha timu.
Akizungmza na Taifa Leo jana, Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Oscar Igaida alisema klabu yake inaweka mikakati kapambe ya kuhifadhi makinda wake wote kwa ajili ya kuwategemea msimu ujao na miaka itakayofuata.
Miongoni mwa makinda wa Leopards ni Ezekiel Owade, Yusuf Mainge, Moses Mburu, Dennis Sikhayi, Michael Kibwage, Victor Mavisi, Clyde Senaji, Jaffery Odeny, Vincent Oburu na Marvin Nabwire ambao kadri ya umri wao ni miaka 22.
Igaida alisema Leopards inajaribu kuiga mpango wa marehemu, James Siang’a ambaye aliunda kikosi cha sasa cha Gor Mahia ambacho kimevuma mfululizo kwa muda mrefu.
Alipochukua usukani mnamo 2009, Siang’a alisajili wachezaji wengi wa umri mdogo na kuomba afisi impe muda wa miaka mintano.
“Tutawahifadhi makinda wetu klabuni kwa manufaa ya baadaye. Tayari viwango vya baadhi yao vimeanza kupanda,” alisema Igaida.
“Wachezaji wetu wengi wana umri mdogo, lakini huenda wakafanya makubwa iwapo watazidi kuimarika jinsi siku zinavyoendelea,” aliongeza.
Hata hivyo, afisa huyo alisema baada ya kusajili nyota wawili mwezi huu, klabu hiyo inapanga kusajili nyota wengine wawili kabla ya muda wa kusajili wachezaji wapya kumalizika.
“Baada ya kukamilisha usajili wetu mwezi huu, tunatarajia kuwa klabu imara zaidi kwenye ligi kuu ya SportPesa Premier League (SPL),” alisema.
Leopards ambayo kwa muda mrefu haijakuwa na mshambuliaji wa kutegemea imemsajili Eugene Mukangula mwenye umri wa miaka 22 kutoka Thika United.
Mukangula ni mshambuliaji matata ambaye amekuwa akiisaidi Thika katika mechi za ligi kuu kabla ya kuuliza ruhusa ya kuondoka baada ya klabu hiyo kushindwa kumlipa mshahara kwa miezi kadhaa.
Straika huyo aliyekubali mkataba wa miaka mitatu anatarajiwa kuiongezea nguvu safu ya ushambuliaji ambayo imekuwa ikimtegemea Ezekiel Odera ambaye amerejea majuzi baada ya kuuguza jeraha kwa wiki kadhaa.
Habari za kuaminika zimesema Ingwe kadhalika inawania kiungo mmoja, kuongezea kwa Saad Musa ambaye alijiunga na mabingwa hao wa GOtv akitokea Thika United.
Musa ambaye zamani alikuwa na Azam Youth na Nairobi City Stars amekubali mkataba wa mwaka mmoja kusaidiana na Wyvonne Isuza ambaye amekuwa akicheza bila kupumzika.
Kadhalika kuna uvumi kwamba huenda beki wa kimataifa wa Uganda Greens, Isaac Isinde akanaswa na Ingwe.
Lakini juhudi za kumsajili straika Elvis Rupia kutoka Nzoia Unitedzilizidi kuambulia patupu.