Iravaya Obiri mambo mazuri kwake Olimpiki kwa wenye ulemavu
Na GEOFFREY ANENE
MKENYA Marion Iravaya Obiri amekuwa na siku nzuri katika mashindano ya Olimpiki kwa watu wenye ulemavu Ijumaa baada ya kushinda mechi tatu katika fani ya bocce mjini Abu Dhabi nchini Milki za Kiarabu.
Chipukizi huyu mwenye umri wa miaka 20 alianza kampeni yake kwa kulemea Keshuv Dabypersad kutoka Mauritius kwa alama 15-0. Alipoteza mechi ya pili 10-7 dhidi ya Tung Tung Lee kutoka Chinese Taipei kabla ya kutesa Bianca Paula Ionita kutoka Romania 9-3 na kukamilisha siku kwa kupepeta Nawaf Abdulkarim Al-Balushi kutoka Oman 12-2.
Katika mpira wa vikapu, matumaini ya Kenya kufanya vyema yalididimia pale ilipokung’utwa 21-16 na Ubelgiji.
Kabla ya hapo Kenya wanaume hawa wa Kenya walikuwa wameandikisha matokeo mseto Machi 14 walipocharaza Algeria 8-0, Chinese Taipei 16-11, Nigeria 8-2 na Luxembourg 9-8 kabla ya kulemewa na Urusi 11-4, Milki za Kiarabu 20-4 na Ivory Coast 7-6.
Kenya iliendelea kutetemesha katika soka pale ilipobwaga India 3-0. Katika mechi yake ya kwanza, Kenya ilizima Marekani 3-2.
Kenya ina washiriki katika soka, mpira wa vikapu, voliboli, voliboli ya ufukweni, handiboli, riadha, ‘bocce’, kuendesha baiskeli, gofu, kuogelea kwenye bwawa na kuogelea katika mto, ziwa ama bahari (Open Water Swimming).