Jadon Sancho acheka na nyavu mara tatu kuiongoza Dortmund kuisagasaga Paderborn 6-1
Na CHRIS ADUNGO
CHIPUKIZI Jadon Sancho alifunga mabao matatu kwa mara ya kwanza tangu kurejelewa kwa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) na kusaidia waajiri wake Borussia Dortmund kuisagasaga limbukeni Paderborn 6-1.
Baada ya vikosi vyote viwili kutoshana nguvu katika kipindi cha kwanza, Thorgan Hazard aliwafungulia Dortmund ukurasa wa mabao kunako dakika 54 kabla ya Sancho kucheka na nyavu kwa mara ya kwanza tangu Februari 29, 2020.
Sancho alifunga bao la pili sekunde chache baada ya penalti ya Uwe Hunemeier kuwafutia Paderborn machozi kunako dakika ya 72. Achraf Hakimi na Marcel Schmelzer walifanya mambo kuwa 5-1 kabla ya Sancho kufunga kazi kwa kupachika wavuni goli lake la tatu mwishoni mwa kipindi cha pili.
Sancho mwenye umri wa miaka 20 ndiye mchezaji wa kwanza mzawa wa Uingereza baada ya miaka 31 kufunga jumla ya mabao matatu katika mechi moja kwenye mojawapo ya Ligi Kuu za Ulaya nje ya Uingereza.
Fowadi wa zamani wa Luton, Brian Stein alikuwa mtu wa mwisho kujivunia ufanisi huo wakati kikosi chake cha Caen kilipokuwa kikivaana na Cannes katika Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) mnamo Mei 1989.
Baada ya kufunga bao lake la kwaza dhidi ya Paderborn, Sancho alivua jezi katika tukio lililochochewa na azma ya kufichua ujumbe wa “Haki kwa George Floyd” aliokuwa ameuandika kwenye sehemu ya ndani ya sare yake.
Floyd aliaga dunia baada ya kudhulumiwa na maafisa wa polisi waliomtia nguvuni nje ya duka mjini Minneapolis, Minnesota mnamo Mei 25, 2020. Ni mauaji ambayo yamechangia maandamano makubwa nchini Amerika.
Alionyeshwa kadi ya manjano kwa hatua hiyo ya kuvua jezi.
Bao la kwanza la Sancho ambaye ni mchezaji wa zamani wa Manchester City lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na Julian Brandt kabla ya kushirikiana tena na Hazard kufunga goli la pili.
Ilikuwa mara ya 17 kwa Sancho ambaye kwa sasa anawaniwa pakubwa na Manchester United, kufunga jumla ya mabao matatu kwenye kivumbi cha Bundesliga.
Katika mchuano mwingine wa Bundesliga, Borussia Monchengladbach waliwapokeza Union Berlin kichapo cha 4-1 na kujikweza hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa jedwali kwa alama 56 sawa na Bayer Leverkusen. Dortmund wanashikilia nafasi ya pili kwa alama 60, saba nyuma ya viongozi Bayern Munich.
Paderborn wangali wanakokota nanga mkiani mwa jedwali kwa alama 19 kutokana na mechi 29 zilizopita. Ni pengo la pointi 12 ndilo linatamalaki kati yao na Union wanaoshikilia nafasi ya 14