JANDONI: Uganda katika mizani raundi ya 16-bora ikianza
Na MASHIRIKA
CAIRO, Misri
MECHI za muondoano za hatua ya 16-bora za AFCON zitaanza rasmi leo Ijumaa hadi Jumatatu katika viwanja mbali mbali ambapo washindi wa mechi hizo watasonga mbele hadi hatua ya robo-fainali.
Uganda Cranes ambayo ndio waliobakia miongoni mwa mataifa ya Afrika Mashariki baada ya Kenya, Tanzania na Burundi kuondolewa mapema watamenyana na Senegal ambayo ndiyo timu bora barani Afrika.
Senegal ilimaliza katika nafasi ya pili baada ya kuibuka na ushindi wa 2-0 na 3-0 dhidi ya Tanzania na Kenya mtawalia na kushindwa 1-0 na Algeria katika mechi za Kundi C.
Katika mechi zingine kali za hatua hiyo ya 16-bora, miamba wawili wa soka barani Afrika, Cameroon na Nigeria watakabiliana jijini Alexandria kesho, Jumamosi, huku wenyeji Misri wakikabana na Afrika Kusini, wakati Ghana ikivaana na Tunisia.
Jumla ya timu nane zimefungasha virago kwa kutolewa katika hatua ya makundi, tatu kati ya hizo zilitingwa mechi zote.
Tanzania ndiyo timu iliyofanya vibaya zaidi katika mashindano hayo kitakwimu, baada ya kufungwa jumla ya magoli nane na kufunga mawili, hivyo wamemaliza wakiwa na uwiano wa magoli sita zaidi ya waliofunga.
Timu inayofuata kwa kufanya vibaya ni Namibia ambayo pia ilifungwa mechi zote na kumaliza na uwiano wa magoli zaidi ya waliyofunga, kisha Burundi yenye alama sufuri pia na uwiano wa magoli zaidi ya waliyofunga.
Timu zingine zilizofungasha virago ni Guinea-Bissau iliyomaliza na pointi moja, Zimbabwe pia pointi moja, Mauritania pointi mbili, Angola pointi mbili na Kenya yenye pointi tatu.
Timu nne zilitinga raundi ya muondoano kama timu bora ambazo ni Guinea, DR Congo, Afrika Kusini na Benin.
Wakati huo huo, aliyekuwa nahodha wa Super Eagles ya Nigeria, Austine Okocha maarufu kama ‘JJ’ amewaonya wachezaji wa kikosi hicho dhidi ya Cameroon zitakapokutana kesho mjini Alexandria.
Nigeria walimaliza katika nafasi ya pili katika Kundi B, nyuma ya Madagascar na sasa watakutana na Indomitable Lions chini ya kocha Clarence Seedorf ambao pia walimaliza katika nafasi ya pili katika Kundi F.
Kujifunza
Okocha, ambaye alikuwa kwenye kikosi kilichoshindwa na Cameroon katika fainali ya 2000 jijini Lagos, amemtaka Gernot Rohr kuhakikisha vijana wake wajifunze kutokana na mechi yao dhidi ya Madagascar ambayo walishindwa na limbukeni hao.
“Nijuavyo, Nigeria wana kibarua kigumu Jumamosi. Cameroon daima wanakuwa wagumu tunapokutana nao mechi inakuwa kama vita,” Okocha alisema.
“Lazima timu yetu ijipange vilivyo kwani lazima mshindi na mshindwa apatikane Jumamosi. Sharti wasahau mechi zilizopita na kuimarisha mchezo wao kwa mtihani mgumu ulio mbele yao.
“Kichapo dhidi ya Madagascar sharti kiwe funzo kwao kabla ya kukutana na Cameroon kwa sababu taifa zima linawategemea. Kwa hakika itakuwa mechi ngumu ambayo kila mtu lazima awe makini daima, wakati huu nchi inasubiri ubingwa wa taji hili,” alisema nyota huyo wa zamani aliyesakatia klabu maarufu nchini Ujerumani na kwenye ligi kuu ya Uingereza (EPL).
Nigeria ni mabingwa wa AFCON wa miaka 1980, 1994 na 2013, na ni miongoni mwa timu zinazopewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa mwaka huu.