Japan yaadhibu Chipu 48-34 katika raga ya dunia ya daraja la pili
Na GEOFFREY ANENE
TIMU ya taifa ya raga ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 20 almaarufu Chipu ilitoa miamba Japan kijasho kabla ya kusalimu amri kwa alama 48-34 kwenye Raga ya Dunia ya daraja la pili Jumatano usiku mjini Sao Paulo nchini Brazil.
Katika mechi hiyo ya mwisho ya Kundi “A”, mabingwa wa Afrika Kenya walipata alama zao kupitia kwa Geoffrey Okwach (miguso miwili) na Hibrahim Ayoo, Timothy Omela Okwemba na Ian Masheti (mguso mmoja kila mmoja) pamoja na penalti na mikwaju mitatu kutoka kwa nahodha msaidizi Dominic Coulson.
Ukilinganisha uzoefu mkubwa ambao Japan inayo ikiwemo kunyakua mataji ya mashindano haya mwaka 2014 na 2017, matarajio hayakuwa makubwa kwa Chipu, ambayo inarejea katika mashindano haya baada ya kuwa nje miaka 10.
Kenya ilianza vibaya pale ilifungwa mguso dakika ya pili kutoka kwa Halatoa Vailea ulioandamana na mkwaju wa Takumi Aoki.
Vijana wa kocha Paul Odera walikata uongozi huo wa alama 7-0 kupitia penalti ya Coulson dakika mbili baadaye.
Coulson alipata fursa nyingine ya kuongeza penalti na kupunguza mwanya huo hadi alama moja dakika ya sita, lakini penalti yake ilikuwa fyongo.
Japan kisha ilitisha kusambaratisha Kenya ilipopachika miguso miwili kupitia kwa Shohei Tsujimura na Taihei Kusaka iliyoandamana na mikwaju kutoka kwa Aoki na kuongoza 19-3.
Mguso bila mkwaju kutoka kwa Ayoo dakika ya 22 ulifufua matumaini ya Kenya kufikia Japan.
Hata hivyo, Japan ilifurahia kuenda mapumzikoni kifua mbele 31-15 baada ya Vailea kupachika miguso miwili, mguso mmoja ulioandamana na mkwaju kutoka kwa Aoki, huku Kenya ikipata mguso kutoka kwa Okwemba uliofuatiwa na mkwaju wake kutoka kwa Coulson.
Chipu ilibabaisha Japan mapema katika kipindi cha pili ilipopunguza mwanya huo hadi 31-29 kupitia kwa miguso ya Masheti na Okwach iliyoandamana na mikwaju kutoka kwa Coulson.
Japan ilipata nafasi ya kupumua 38-29 Chipu ilipoadhibiwa kwa mguso ulioandamana na mkwaju. Kenya ilijikakamua na kupunguza pengo hilo hadi 38-34 kupitia mguso wa Okwach ulioandamana na mkwaju kutoka kwa Okwach.
Hata hivyo, huo ndio umbali Kenya ilifika kwani Japan ilifunga miguso miwili kutoka kwa Aoki na Futo Yamaguchi ikinufaika na wachezaji wawili wa Kenya kuonyeshwa kadi ya njano na kumaliza mechi watu 13.
Wakenya sasa watamenyana na Canada katika mechi ya kutafuta nambari tano na sita.
Canada ilikuwa katili katika mechi yake ya mwisho ya Kundi B ilipolipua Hong Kong 78-26 baada ya kuongoza 38-14 wakati wa mapumziko. Kenya na Canada zilimaliza mechi zao za makundi katika nafasi ya tatu kwa alama tano na saba, mtawalia.
Ureno ilitawala Kundi B baada ya kucharaza Tonga 40-3 katika mechi ya timu mbili za kwanza za kundi hilo. Wareno watakabiliana na Wajapani katika fainali Julai 21 kuamua nani kati yao ataingia Raga ya Dunia ya daraja ya juu mwaka 2020.
Kujaza pengo
Mshindi wa Raga ya Dunia ya daraja la pili kati ya Ureno na Japan atajaza nafasi ya Scotland iliyotemwa kutoka daraja la juu ilipovuta mkia Juni 22.
Tonga itapepetana na Uruguay iliyomaliza Kundi A katika nafasi ya pili.
Mshindi wa mchuano huu atanyakua medali ya shaba.
Uruguay ilikamilisha mechi za makundi kwa kuaibisha wenyeji Brazil 52-10.
Hong Kong na Brazil, ambazo zilikamilisha mechi za makundi kwa kupoteza mechi zote tatu, zitalimana kuamua atakayemaliza katika nafasi ya saba na mkiani.
Kenya ilianza mashindano haya kwa kupoteza 63-11 Julai 9 kabla ya kujinyanyua na kulaza Brazil 26-24 na kisha kukubali kichapo cha 48-34 kutoka kwa Japan.