JUDITH OSIMBA: 'De Gea' wa Harambee Starlets U-20
Na PATRICK KILAVUKA
MNYAKAJI Judith Osimba, 18, hushangaza wengi kutokana na miondoko ya unyakaji boli mithili nyani au kuipangua.
Mnyakaji huyu akiwa langoni, timu hesabu kwamba ngome iko ngangari na huwa komeo halisi langoni kwani, si rahisi nyavu kutikisa kihivihivi.
Isitoshe, huwa sawa na kamanda wa jeshi aliye radhi kudhibiti mashambulizi au uviziaji wowote kwa kutambua kwamba, masihara hayafanyiwi kwenye lango wala katika msambamba.
Kipa Osimba alijitosa katika fani ya kabumbu akiwa miaka kumi na moja.
Anasema amewahi kuwakilisha Shule yake ya Msingi ya St Johns Jogoo road, Nairobi katika mashindano ya michezo ya shule za msingi hadi kiwango cha Nairobi Metropolitan (Tawi la Nairobi zama hizo) kwa miaka mitatu mtawalia 2012, 2013 na 2014 kisha ndoano ya Shule ya Upili ya Nyakach, Kisumu ikamnasa na kuichezea .
Kando na kuichezea shule, mdakaji huyu alikuwa pia mchezaji wa kutegemewa sana katika timu ya mtaani ya Under-10 ya Masabets, Nyakach chini ya kocha Elvis Wafula ambayo aliidakia akiwa nyumbani.
Mwaka 2018, alidhihirisha yeye si michache baada ya kuifikisha timu ya Pluto Queens kwenye fainali za kitaifa katika mashindano ya Chapa Dimba na hata kutawazwa kipa bora wa patashika hilo ambalo liliandaliwa uwanja wa Bukhungu, Kaunti ya Kakamega.
Pia, nyota yake jaha ilingara katika kindumbwendumbwe cha Timu Wanyonyi Super Cup akiichezea timu ya Patriots Queens na akatuzwa pia kama mlinda lango mahiri zaidi na kutunukiwa kikombe. Alikubali tu magoli mawili kimiani katika fainali yao dhidi ya Kabete Chic ambao waliiobuka mabingwa.
Kulingana na kocha Joseph Odhiambo aliyeshikilia mikoba ya timu ya Queens, Kipa huyu ni mchezaji anayeamakinika sana mchumani na ana bidii ya mchwa katika kufanya mazoezi na kujituma sana wakati wa mapambano hali ambayo iliifikisha timu fainali na hata jasho lake kutambuliwa na wadau waandalizi wa dimba hilo.
Osimba anasema kwamba, kuwa mchezaji wa kandanda kulimfungulia milango ya masomo kwani amefadhili elimu ya sekondari na akamaliza mwaka jana na sasa ana matarajio ya kuvuka ughaibuni milango ya mdhamini wake Catherine Gjeslric ikifunguka, ataenda kwa majaribio.
Hata hivyo, angependa kusakatia timu ya Gaspo ambayo inashiriki ligi ya Primia ya Shirikisho la Soka Kenya (FKF), Akinadada.
Osimba pia amedakia timu ya U-20 ya Harambee Starlets na kutalii nayo katika michuano waliopiga Botswana, Ethiopia na Ghana.
Kipa anayempelekea kuvuta rada ya soka ni David De Gea wa Manchester United kutokana na mahanjam yake ya kunyaka boli na kudhibiti lango.
Siri yake katika fani hii? Asema ni kuwa na nidhamu na kutia bidii mazoezini na kufuata mawaidha ya mkufunzi wake.