Michezo

Juventus kumtia Ramsey mnadani

June 13th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

JUVENTUS wamefichua mpango wa kuzinadi huduma za kiungo Aaron Ramsey mwishoni mwa msimu huu baada ya kukiri kwamba wameanza kulemewa na ukubwa wa gharama ya kumdumisha kimshahara.

Ramsey ambaye ni mzawa wa Wales, aliingia katika sajili rasmi ya Juventus mnamo Februari 2019 baada ya kuagana na Arsenal bila ada yoyote.

Mshahara wake kwa sasa katika mkataba wa miaka mitano unaotarajiwa kutamatika mwishoni mwa 2023, ni kima cha Sh56 milioni kwa wiki.

Huku vikosi vingi vya bara Ulaya vikipania kubana hazina zao za fedha baada ya bajeti kulemazwa na janga la corona, Juventus wana ulazima wa kupunguza gharama yao ya matumizi.

Kati ya klabu za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) zinazopigiwa upatu wa kujitwalia huduma za Ramsey iwapo atahiari kupunguziwa ujira wa kila mwezi ni Manchester United na Tottenham Hotspur ambao wako radhi kuweka mezani kima cha Sh5 bilioni. Ingawa hivyo, Juventus wametangaza kuwa watakuwa radhi kumwachilia kiungo huyo kwa kima cha Sh8 bilioni kuanzia mwisho wa mwezi ujao.

Licha ya kutia saini mkataba wake na Juventus mnamo Februari 2019, Ramsey ambaye pia ni nahodha wa timu ya taifa ya Wales alitua jijini Turin mnamo Julai 2019 baada ya muda wa kuhudumu kwake uwanjani Emirates kutamatika rasmi.

Japo alifungia Juventus mabao mawili katika mechi mbili za Ligi Kuu ya Italia (Serie A) mwanzoni mwa Machi 2020 Ramsey amekuwa mwepesi wa kupata majeraha, tukio ambalo linatrajiwa kumchochea kocha Maurizio Sarri kumtia mnadani.

Sogora huyo amewajibishwa na Juventus mara tisa pekee hadi kufikia sasa muhula huu. Juventus wanawania taji la tisa mfululizo la Ligi Kuu ya Serie A.

Kampeni za Serie A zitarejelewa mnamo Juni 20 huku Juventus wanaoselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 63 wakiratibiwa kuvaana na Bologna ugenini mnamo Juni 22.