Michezo

Kamworor na Jepkosgei wasema wanalenga juu zaidi 2018

March 27th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

MFALME wa Riadha za Nusu-Marathon Duniani, Geoffrey Kamworor na mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 21 za wanawake Joyciline Jepkosgei wametangaza mipango yao ya mwaka 2018 baada ya kurejea nchini Jumatatu usiku.

Kamworor, ambaye alishinda taji la dunia kwa mara ya tatu mfululizo Machi 25, amesema atashiriki mbio za mita 5,000 na mita 10,000 kwenye Riadha za Diamond League kujipiga msasa kabla ya kutetea taji lake la New York City Marathon nchini Marekani mnamo Novemba 4, 2018.

Jepkosgei, ambaye alipoteza taji lake la Valencia Half Marathon baada ya kumaliza nyuma ya Muethopia Netsanet Gudeta Kebede, amesema atalenga kuvunja rekodi yake ya dunia ya saa 1:04:51.

Timu ya riadha ya Kenya baada ya kutua uwanjaji JKIA Jumatatu usiku. Picha/ Geoffrey Anene

Mjini Valencia hapo Machi 25, Kamworor, ambaye alinyakua mataji ya mwaka 2014 mjini Copenhagen nchini Denmark na mwaka 2016 mjini Cardiff nchini Wales, alinyakua taji lake la tatu kwa saa 1:00:02.

Mzawa wa Kenya, Abraham Cheroben, ambaye ni Mbahraini na bingwa wa Valencia Half Marathon mwaka 2014, 2015 na 2017, alimaliza katika nafasi ya pili (1:00:22) naye raia wa Eritrea Aron Kifle akafunga tatu-bora (1:00:31).

Wakenya Leonard Barsoton (1:01:14), Barselius Kipyego (1:01:24) na Jorum Lumbasi (1:01:34) walimaliza katika nafasi za 12, 15 na 18, mtawalia.

Gudeta alivunja rekodi ya mzawa wa Kenya, Mholanzi Lorna Kiplagat ya Nusu-Marathon Duniani ya wanawake pekee ya saa 1:06:25 baada ya kushinda kwa saa 1:06:11.

Kabla ya mbio, Kiplagat alikuwa amebashiri rekodi yake itafutwa. Jepkosgei alikamilisha kwa saa 1:06:54, sekunde mbili mbele ya Mkenya mwenzake Pauline Kaveke.