Kayaba Youth waapa kubeba taji la KYSD
Na JOHN KIMWERE
TIMU ya Kayaba Youth Sports Academy (KYSA) ni kati ya vikosi vipya vinavyoshiriki kampeni za kuwania Ligi ya KYSD kwa wasiozidi umri wa miaka 12 muhula huu. KYSA inayotiwa makali na kocha, Emmanuel Kelvin Omanyo imepania kujituma mithili ya mchwa kuhakikisha inabeba taji hilo.
”Bila shaka nina imani tosha chipukizi wangu watafanya kazi nzuri na kutwaa taji hilo,” kocha huyo alisema na kuongeza kuwa amepanga wachezaji wazuri ambao wamegundua wana uwezo wa kuvuruga wapinzani wao na kutenda kweli.
Hata hivyo anasema anafahamu timu zote 18 zimejipanga kupigania taji hilo ambapo kamwe hawawezi kudharau wapinzani wao.
FULL TIME RANGERS
Kando na KYSA orodha ya timu mpya inajumuisha: Orodha ya washiriki wapya inajumuisha Biira Sports Academy kutoka Mbotela, Full Time Rangers kutoka City Cotton, Blue Bentos kutoka Umoja, Young Lions pia kutoka Kaloleni na Arizen Soccer Academy kutoka Mukuru kwa Reuben.
YOUNG ELEPHANT
Katika mpango mzima anadokeza kuwa kunazo timu kadhaa zinazomtia hofu kiasi ingawa yupo tayari kupambana mwanzo mwisho kupigania taji hilo.
Ametaja timu hizo kama Kinyago United mabingwa watetezi, Sharp Boys, Young Elephant inayoongoza kwenye jedwali kwa alama 12 baada ya kushinda zote nne ambazo imeshiriki. Nayo KYSA chini ya nahodha Quinton Mokaya inafunga tano bora kwa kuzoa alama tisa bada ya kushinda mechi nne na kupoteza moja dhidi ya Young Elephant.
AFRICAN SPORTS (TANZANIA)
Kocha huyo anasema kuwa analenga kumaliza mechi za mkumbo wa kwanza katika nafasi mbili za kwanza ili kumaliza kazi kwenye mechi za raundi ya pili.
KYSA ilianzishwa mwaka 2010 nia kuu ikiwa kukuza talanta za wachezaji chipukizi katika maeneo ya mabandani. ”Nina imani tosha endapo tutapata ufadhili vizuri tumekaa vizuri kupalilia makucha ya chipukizi wengi na kuibuka wachezaji wa kimataifa miaka ijayo,” alisema na kuongeza kuwa ukosefu wa ufadhili kwa timu nyingi zinazopatikana katika mitaa ya mabanda huchangia wachezaji wengi kutotambuliwa.
Kocha huyo alianza kushiriki soka akichezea timu ya Fisa FC baada ya kukamilisha masomo ya Shule ya Pili. Pia anajivunia kusakatia Busia United mwaka 2013 ilipokuwa ikishiriki kipute cha Supa Ligi ya Taifa (NSL), GFE 105 Eldoret na Fortune FC.
Pia aliwahi kuchezea African Sports, Mbaghala Market na Muheza United zote za Tanzania.