Michezo

KCB yatwaa huduma za Munala kunoa kikosi cha voliboli

December 8th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

BENKI ya KCB imeteua kocha mkuu wa timu ya taifa ya voliboli ya Kenya na klabu ya Kenya Pipeline, Japheth Munala kuwa kocha mpya wa klabu ya KCB mnamo Ijumaa.

Munala, ambaye aliwahi kunoa klabu hii ya wanawake ya KCB kati ya mwaka 2008 na 2011 kabla ya kujiunga na Pipeline, amerejea ‘nyumbani’ akiandamana na wachezaji saba wapya.  Wachezaji hao ni Violet Makuto, Noel Murambi, Leonida Kasaya, Jemima Siangu, Christine Njambi, Veronica Kilabat na Truphosa Chepkemei.

“Benki ya KCB imeteua Japheth Munala kuwa kocha mpya mkuu wa timu ya voliboli ya KCB. Uteuzi huu, ambao unaanza Desemba 5, 2018, umeshuhudia pia wachezaji saba wapya wakiungana nasi. Mageuzi haya yanalenga kuimarisha matokeo yetu msimu ujao,” KCB imesema katika taarifa kwa vyombo vya habari.

Munala anawasili baada ya kuongoza Pipeline kunyakua mataji ya Ligi Kuu mwaka 2014, 2015, 2016 na 2017. Mwaka 2018, Pipeline ilikamilisha katika nafasi ya tatu nyuma ya mabingwa wapya Kenya Prisons na nambari mbili KCB, ambayo ilikuwa chini ya kocha Vernon Khainga.

Kwa kumaliza ligi katika nafasi ya pili, KCB ilifuzu kupeperusha bendera ya Kenya katika Klabu Bingwa Afrika mwaka 2019. Itawakilisha Kenya katika kipute hicho nchini Misri pamoja na mabingwa wa zamani wa Afrika, Prisons.

Mlezi wa klabu ya voliboli ya KCB, Judith Sidi Odhiambo amesema kwamba mabadiliko haya yote yanalenga kuipa nguvu kwa mashindano ya mwaka 2019.

 “Tunafurahia kurejesha Munala katika klabu ya KCB. Tunatumai kunufaika na ujuzi wake, mtindo wake na falsafa yake ya voliboli kuwezesha klabu hii kupiga hatua mbele katika mashindano ya Kenya, Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na Bara Afrika,” alisema Odhiambo, ambaye ni mmoja wa maafisa wakuu wa KCB.

Kuwasili kwa wachezaji saba wapya kutashuhudia KCB ikitema wachezaji wanane mwisho wa mwezi huu wa Desemba. Munala atasaidiwa na David Kinga (Naibu Kocha), mchezaji wa timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande Philadelphia Olando (kocha wa mazoezi ya viungo) na daktari Simon Kibe.

Klabu ya KCB ni mabingwa mara saba wa Afrika Mashariki na Kati na malkia wa Afrika mwaka 2006.