Michezo

Kenya sasa nambari 111 duniani viwango vya soka

May 17th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

HARAMBEE Stars ndiyo timu pekee kutoka eneo la Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) iliyoimarika kwenye viwango bora vya soka duniani, Alhamisi.

Viwango hivi vipya vimetangazwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), huku Kenya ikipaa kutoka nafasi ya 113 hadi nambari 111.

Stars imenufaika pakubwa na Zimbabwe na Madagascar kuteremka nafasi tatu kila mmoja hadi nambari 113 na 114, mtawalia.

Katika eneo la Cecafa, Uganda imesalia katika nafasi ya 74 duniani. Kenya ni ya pili (imeimarika kutoka 113 hadi 111) nazo Rwanda, Sudan na Tanzania zimesalia katika nafasi za 123, 126 na 137 duniani, mtawalia.

Ethiopia na Burundi zimeshuka nafasi moja kila mmoja hadi nambari 146 duniani. Sudan Kusini imeteremka nafasi mbili hadi nambari 157 duniani nayo Djibouti imekwamilia nafasi ya 198. Eritrea na Somalia zinavuta mkia katika nafasi ya 207 duniani.

Tunisia ndiyo nambari moja Afrika. Inashikilia nafasi ya 14 duniani. Senegal, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Morocco, Misri na Nigeria zinafuatana katika nafasi za 28, 38, 42, 46 na 47 duniani, mtawalia.

Cameroon na Ghana zimeruka juu nafasi moja hadi nambari 50 duniani nayo Burkina Faso iko chini nafasi moja hadi nambari 54 duniani. Cape Verde imesalia katika nafasi ya 58 duniani nayo Algeria inafunga 10-bora Afrika na katika nafasi ya 64 duniani. Algeria imetupwa chini nafasi mbili.

Hakuna mabadiliko katika nafasi 47 za kwanza duniani, huku Ujerumani, Brazil, Ubelgiji, Ureno, Argentina, Uswizi, Ufaransa, Uhispania, Chile na Poland zikiwa ndani ya mduara wa 10-bora, mtawalia.