Michezo

Kenya tayari kuandaa mashindano ya dunia ya Taekwondo

Na TOTO AREGE November 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KENYA sasa iko tayari kuandaa mashindano ya Dunia ya Taekwondo ya vijana chini ya miaka 21, ambayo yatafanyika kati ya Disemba 3 hadi Disemba 6 mwezi ujao,  katika Uwanja wa Ndani wa Kasarani, Nairobi.

Timu ya Kenya itajumuisha wachezaji 16 (nane wa kike na nane wa kiume). Zaidi ya mataifa 80 tayari yamedhibitisha  kushiriki mashindano hayo.

Akizungumza katika kikao na wanahabari jijini Nairobi jana, Rais wa Shirikisho la Taekwondo la Kenya (KTF) Meja (Rtd) Suleiman Sumba aliangazia utayari wa Kenya na ajenda kuu ikiwa ni kupanda miti bilioni 15 kufikia 2032.

“Kenya iko tayari. Mashindano haya chini ya kauli mbiu  ‘Hatua ya Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi”  kunaonyesha kwamba michezo inaweza kuwa kichocheo cha ufahamu wa mazingira,” alielizea Meja Sumba.

Shirikisho hilo mwezi uliopita lilizindua mpango kabambe wa upandaji miti uliopewa jina #KenyaYetuMsituWetu ambao unalenga kupanda miti 11,000.

Aidha alifichua kwamba kikosi cha wachezaji 16 cha Timu ya Kenya tayari kiko kambini. Kikosi hicho hicho, kinatarajiwa kusafiri kuelekea Abidjan, Côte d’Ivoire ambapo watafanyia mazoezi kabla ya kurejea nchini kwa mashindano hayo.

Michuano hiyo itawaleta pamoja zaidi ya wanariadha 1,000, makocha na maafisa kutoka takribani nchi 140 zikiwemo Korea Kusini, Urusi, Israel, Brazil, Misri, Nigeria, Afrika Kusini.

“Michuano hii ni mfano wa kukua kwa Kenya katika usimamizi wa michezo duniani; inasisitiza dhamira ya serikali kuweka michezo kama chombo cha maendeleo ya vijana, ukuaji wa uchumi, na utunzaji wa mazingira,” Jackson Munywoki Afisa Mkuu wa Michezo katika wizara ya michezo.

Timu hiyo ya Kenya imekuwa ikijifanyia mazoezi katika Ukumbi wa Phoenix, Kahawa 44, kabla ya kuondoka kwenda Abidjan.

Kikosi cha timu ya Kenya

Wanaume

Williams Odhiambo

David Mbuguwe

Elvis Omondi

Lesley Aure

Clay Mukoko

Geroge Williams

Festo Mbalala

Frank Thomas

Mabinti

Stacy Dock

Selina Zenna

Bridgit Lucy

Wendy Trina

Walda Mullah

Cecilia Wangui

Sophy Clay