Kenya yaburuta mkia London Sevens
Na GEOFFREY ANENE
KENYA imevuta mkia kwenye duru ya tisa ya Raga ya Dunia jijini London nchini Uingereza baada ya kuchapwa na Japan 26-17 katika nusu-fainali ya kuorodheshwa kutoka nafasi ya 13 hadi 16, Jumapili.
Shujaa sasa iko katika nafasi ya 14 kwa alama 27 na katika hatari zaidi ya kutemwa kutoka ligi hii ya kifahari inayojumuisha mataifa 15 na timu moja alikwa katika duru 10.
Imerukwa na Wales ambayo imezoa alama tano kutoka jijini London na kufikisha alama 29 ikisalia duru ya Paris pekee nchini Ufaransa hapo Juni 1-2 msimu huu ukatike.
Vijana wa kocha Paul Murunga waliingia duru ya London Sevens wakiwa katika nafasi ya 13 kwa alama 26, moja mbele ya Wales na nne juu ya Japan, ambayo imesalia katika nafasi ya 15, lakini imepunguza mwanya wa alama kati yake na Kenya hadi mbili baada ya kuduwaza wenyeji Uingereza 29-14 katika fainali ya nambari 13.
Baada ya kusajili matokeo mseto katika mechi za makundi katika siku ya kwanza pale walipokung’utwa na Fiji 24-17 na Ufaransa 31-17 na kulima Samoa 21-20 Mei 25, Kenya iliona cha mtema kuni Jumapili.
Ilianza siku ya pili kwa kuchapwa 29-21 dhidi ya Scotland katika robo-fainali ya kuorodheshwa kutoka nambari 9-16 almaarufu Challenge Trophy kabla ya kuzimwa na Japan 26-17 katika nusu-fainali ya kutafuta nambari 13-16.
Andrew Amonde alifunga miguso miwili dhidi ya Scotland naye Jeffery Oluoch akachangia mguso mmoja. Bush Mwale alipachika miguso miwili dhidi ya Japan, huku Oluoch akifunga mguso mmoja.
Duru ya London Sevens ilitamatika Jumapili usiku.Â