Michezo

Kenya yaimarika hadi nafasi ya 105 viwango vya FIFA

March 16th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

KENYA iko katika orodha ya mataifa 14 kutoka Bara Afrika yaliyoimarika kwenye viwango vipya vya ubora vya soka duniani.

Mabingwa hawa wa Afrika Mashariki na Kati wameruka juu nafasi moja na kutulia katika nafasi ya 105 duniani.

Burkina Faso na Cape Verde pia wamepaa nafasi moja hadi nambari 56 na 61, mtawalia.

Mali wamerukia nafasi ya 67 kutoka 69, Afrika Kusini wako juu nafasi moja hadi nambari 76, Congo Brazzaville wamepaa kutoka 88 hadi 87 nao Msumbiji wameimarika kutoka 107 hadi 105.

Rwanda wako juu nafasi mbili hadi nambari 112, Sudan, Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) na Malawi wamepaa nafasi moja kila mmoja hadi nambari 117, 121 na 123, mtawalia.

Burundi, Lesotho na Ushelisheli wako juu nafasi moja hadi nambari 142, 144 na 191, mtawalia.

Tunisia (23 duniani), Senegal (27), Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (39) na Morocco (42) wamesalia katika nafasi nne za kwanza barani Afrika. Misri ni ya tano barani Afrika na 44 duniani baada ya kuteremka nafasi moja. Cameroon, Nigeria na Ghana hazijasonga kutoka nafasi za 51, 52 na 54 duniani, mtawalia.

Katika eneo la Cecafa, Uganda inaongoza katika nafasi ya 78 duniani. Inafuatwa na Kenya (105 duniani), Rwanda (112), Sudan (117), Ethiopia (imeteremka nafasi mbili duniani hadi nambari 137), Burundi (142), Tanzania (imesalia 146), Sudan Kusini (imeshuka nafasi moja hadi nambari 154) nazo Djibouti, Eritrea na Somalia zimesalia katika nafasi za 187, 206 na 206, mtawalia.

Ndani ya mduara wa 10-bora duniani, Ujerumani Brazil, Ureno, Argentina na Ubelgiji zimekwamilia nafasi tano za kwanza, huku Poland ikiruka juu nafasi moja na kutua nambari sita. Uhispania, Uswizi, Ufaransa na Chile zinafunga 10-bora katika usanjari huo. Italia, Uingereza na Uholanzi zinashikilia nafasi za 14, 16 na 21, mtawalia.