• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 4:54 PM
Kenya yainyeshea Sudan 4-0 U-17

Kenya yainyeshea Sudan 4-0 U-17

Na GEOFFREY ANENE

KENYA imeanza soka ya kufuzu kushiriki mashindano ya Afrika kwa wachezaji wa kiume wasiozidi umri wa miaka 17 kwa kupepeta Sudan Kusini 4-0 uwanjani Azam Complex mjini Chamazi jijini Dar es Salaam, Tanzania, Jumanne.

Vijana wa kocha Michael Amenga wamebusu nyavu za Sudan Kusini kupitia mabao ya Keith Imbali, Mathew Malisau Mwendwa, Telvin Irungu Maina na penalti kutoka kwa Nicholas Ochieno.

Kenya ilipata bao la kwanza kupitia shuti la mguu wa kushoto kutoka kwa Imbali dakika ya 12 baada ya safu ya ulinzi ya Sudan Kusini kuzembea.

Malisau aliongeza bao la pili dakika ya 61 akichota mpira msafi juu ya kipa baada ya mchezaji wa Kenya kupokonya mchezaji wa Sudan Kusini mpira katikati ya uwanja pembeni kushoto.

Mambo yaliharibika zaidi katika kambi ya Sudan Kusini pale wasiwasi katika safu ya ulinzi ulitunuku Kenya nafasi nyingine murwa ya kuimarisha magoli yake kupitia Irungu dakika ya 76.

Ochieno alihitimisha maangamizi haya kwa kupiga kwa ustadi penalti iliyopatikana dakika ya 90 baada ya mchezaji wa Sudan Kusini kuvuta Mkenya Richdonald Bolo ndani ya kisanduku akitaka kupiga mpira.

Baada ya ushindi huu, Kenya inaongoza Kundi A kwa alama tatu sawa na Sudan Kusini na Ethiopia zilizobwaga Djibouti 2-1 na Uganda 1-0 Agosti 12, mtawalia.

Rwanda inaongoza Kundi A kwa alama sita baada ya kubwaga Sudan 3-1 hapo Agosti 11 na Burundi 4-3 Agosti 13.

Wenyeji wa mchujo huu wa eneo la Afrika Mashariki na Kati, Tanzania, ambao pia wataandaa Kombe la Afrika mwaka 2019, wana alama tatu baada ya kulemea Burundi 2-1 Agosti 11.

Ratiba ya Kenya:

Kenya 4-0 Sudan Kusini (Agosti 14, Chamazi)

Djibouti na Kenya (Agosti 17, Chamazi)

Kenya na Uganda (Agosti 19, Uwanja wa Taifa)

Ethiopia na Kenya (Agosti 22, Chamazi)

You can share this post!

Ombi la Gor kusongeshewa mechi KPL lakataliwa

Kerr achemka kusikia Innocent Wafula anapania kumtoroka

adminleo