Kibarua Ingwe ikigaragazana na ‘wadosi’ Wazito
Na CECIL ODONGO
KIVUMBI kikali kinatarajiwa leo Jumamosi katika uga wa Bukhungu mjini Kakamega pale AFC Leopards itakapochuana na mabwanyenye Wazito FC kwenye mechi ngumu ya Ligi Kuu ya Kenya (KPL).
Mechi hiyo tayari imejaa mihemko baada ya mashabiki wa timu zote mbili kuvamiana mtandaoni, wale wa Wazito wakikejeli wapinzani wao kutokana na matatizo ya kifedha yanayowakumba nao mashabiki wa Ingwe wakiapa kutwaa ushindi kwenye mtanange huo licha ya utajiri wa wapinzani wao.
Akizungumza na Taifa Leo, Mwenyekiti wa mabingwa hao mara 13 wa KPL Dan Shikanda, alitaja Kakamega kama kitovu cha ushabiki wa Ingwe na kuwataka mashabiki wajaze uwanja huo kushuhudia timu yao ikipapurana na Wazito FC.
“Ningependa kuwaomba mashabiki wetu kutoka Kakamega na maeneo mengine ya Magharibi mwa nchi kufika uwanja wa Bukhungu ili kushuhudia namna tunavyowadhalilisha Wazito. Ingwe sasa hivi inacheza soka ya kumezewa mate na lengo letu leo ni kupata ushindi,” akasema Shikanda.
Afisa huyo alifunguka na kusema vijana wa Ingwe walicheza soka ya kuvutia dhidi ya Kariobangi Sharks wikendi jana na amejawa na matumaini tele kwamba leo wataendeleza mtindo huo na kutamba.
Wazito ambao walinunua wachezaji kwa hela nyingi zaidi msimu wa uhamisho nao wanatarajia kikosi chao ghali kitawapa ushindi wao wa kwanza kwenye KPL baada ya kupandishwa ngazi msimu jana.
Wanajeshi uwanjani
Mtanange mwingine ambao utakuwa wa kumezewa mate ni kati ya mabingwa wa KPL mwaka wa 2008 Mathare United na wanajeshi Ulinzi Stars walioshinda taji hilo mara ya mwisho mwaka wa 2010 katika uga wa Kenyatta mjini Machakos.
Ulinzi wanaoshikilia nafasi ya pili watalenga kuchupa hadi kileleni mwa KPL kwa kutwaa ushindi huku Mathare United inayonolewa na Salim Ali ikipigania ushindi wake wa kwanza tangu mkufunzi huyo arithi mikoba ya ukocha kutoka kwa Francis Kimanzi.
Limbukeni Kisumu All Stars maarufu kama ‘Otenga’ ambao hawajashinda mechi yoyote tangu wapandishwe ngazi KPL, nao watakuwa katika uga wa Moi, Kisumu kuvaana na Nzoia Sugar FC.
Otenga walipata sare tasa dhidi ya KCB wikendi jana na watapigania ushindi leo ili kupaa kutoka nambari 16 wanayoshikilia kwenye msimamo wa jedwali la KPL.
Nzoia ambao wanashikilia nafasi ya 13 pia bado hawajapata ushindi baada ya kuchapwa 2-1 ugani Sudi wikendi iliyopita na SoNy Sugar FC.