Kibarua sasa ni maandalizi baada ya McCarthy kutaja kikosi cha CHAN
BAADA ya kutaja kikosi cha muda cha wachezaji 30 kwa Kombe la Afrika la wanasoka wanaoshiriki ligi za nyumbani (CHAN 2024), macho yote sasa yapo kwa maandalizi ambayo wenyeji Kenya wataweka ili kung’aa katika dimba hilo.
Kenya, Uganda na Tanzania watakuwa wenyeji wa dimba hilo litakaloanza Agosti 2 hadi 30.
Kenya itakuwa mwenyeji wa mechi zake za Kundi A katika uwanja uliokarabatiwa wa MISC Kasarani unaoweza kusitiri mashabiki 55,000.
Harambee Stars wapo Kundi A pamoja na mabingwa 2018 na 2020 Morocco, mabingwa wa 2009 na 2016 Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Angola na Zambia.
Kama sehemu ya maandalizi yao, Harambee Stars watashiriki kipute cha Mashirikisho ya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kati ya Julai 24-Julai 27.
Kipute cha CECAFA kitakajumuisha mataifa manne ambayo Kenya, Uganda, Sudan Kusini na wenyeji Tanzania.
Kenya itavaana na Tanzania Julai 24 katika uwanja wa Karatu saa kumi jioni, baada ya Uganda kuchuana na Sudan Kusini uwanjani humo kuanzia saa saba mchana.
Washindi watakutana kwenye fainali Julai 27 pamoja na timu ambazo zitamaliza nambari tatu na nne.
Baada ya mechi hizo za CECAFA Stars watarejea nchini kujiandaa kwa mechi yao ya ufunguzi wa CHAN mnamo Agosti 3 dhidi ya DR Congo katika uwanja wa Kasarani.
Difenda wa Gor Mahia, Alphonce Omija, ambaye yupo kwenye orodha aliyotoa McCarthy hapo Jumatano alitoa wito kwa wenzake wasiangazie ugumu wa kundi hilo bali maandalizi mazuri ambayo ndiyo yatawafanya kushinda mechi zao.
“Kila mkosoaji tayari amesema sisi ni dhaifu kwa sababu tumewekwa na wapinzani wagumu. Sisi tutamakinikia maandalizi yetu ili tushinde mechi dhidi ya hao wapinzani wanaosemekana ni wagumu,” alihoji Omija, 22. ambaye amewahi kucheza soka ya kulipwa nchini Oman.
“Kile tutafanya uwanjani ndicho kitakuwa muhimu wala si chambuzi za nani rahisi na nani mgumu. Maandalizi mazuri ndiyo siri ya ufanisi,” akaongeza beki huyo katika mahojiano na Taifa Spoti.
Kocha mzoefu Bob Oyugi naye alisema hatua ya McCarthy kujumuisha wanasoka wengi chipukizi katika kikosi hicho cha kwanza ni hatua nzuri kuhakikisha Harambee Stars inafanya vyema CHAN.
Pia alisema wanasoka wachanga waking’aa wataonekana na maajenti wa klabu za hadhi za kimataifa na hivyo kupata fursa ya kukuza vipaji vyao ng’ambo.
“Kikosi ni kizuri na nina hakika tunaweza kupata wachezaji 11 bora wa kututambisha kwenye mashindano haya,” akasema Oyugi jana.