Michezo

Kigonya aishangaa Sofapaka kumnyima barua licha ya kandarasi kukatizwa

October 24th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na CECIL ODONGO

ALIYEKUWA mnyakaji wa Sofapaka Mathias Kigonya ameulaumu uongozi wa Sofapaka kwa kukataa kumpa barua ya kuondoka, wiki moja baada ya kukatiza rasmi kandarasi yake na mabingwa hao wa KPL mwaka wa 2009.

Kigonya ambaye ni raia wa Uganda aliwakimbia Sofapaka kutokana na sababu za kibinafsi na sasa anasema hana jingine ila kutafuta ujira kwingine ingawa kikwazo kikuu anachokumbana nacho ni kukosa kukabidhiwa barua hiyo muhimu na waajiri wake wa zamani.

“Sina shida kurejea kusakatia klabu nyingine katika ligi ya KPL ila tatizo kuu kwangu ni Sofapaka kukataa kunipa barua ya kuondoka ndipo niweze kupata timu nyingine,” akasema nyani huyo aliyefungia Sofapaka mabao manne kupitia mikwaju ya penalti msimu uliotamatika wa 2017/18.

Hata hivyo taarifa zimeibuka kwamba kilichochangia Kigonya kuagana na ‘Batoto ba Mungu’ ni kukosa kuafikiana kuhusu kandarasi mpya.

Ingawa hivyo, kipa huyo amefichua kwamba anazingatia ofa alizowasilishiwa kutoka klabu mbalimbali ndani na nje ya nchi kabla ya kuamua na kutangaza timu mpya atakayodakia msimu ujao.