Michezo

Kingstone FC mabingwa wapya Koth Biro

August 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN KIMWERE

KINGSTONE FC imeibuka mabingwa wa mashindano ya Koth Biro makala ya 41 chini ya udhamini wa SportPesa iliponyuika Allin Jua Kali FC magoli 7-6 kupitia mipigo ya matuta katika fainali iliyopigiwa Ugani Umeme Ziwani, Nairobi.

Kingstone FC ilinasa ushindi huo baada ya kutoka nguvu mabao 2-2 muda wa kawaida. Mechi ilianza kwa presha tele huku pande zikiwinda taji hilo kwa udi na uvumba. Dakika ya 20, Allin Jua Kali ilipata bao la kwanza kupitia Evans Juma kabla ya Kelwish Walubukha kusawazishia Kingstone dakika 19 baadaye.

Kipindi cha pili, Chrispinus Onyango alitingia Kingstone FC kabla ya Allin Jua Kali kusawazisha kupitia Walcott Walla dakika ya 68. Wafungaji wa mikwanju ya penalti ya Kingstone walikuwa Maina Hussein, Waka Nelson, Oreso Kevin, Eugene Oduor, Brian Ochieng, Juma Casillas na Muriithi Christopher.

Nayo Allin Jua Kali ilitingiwa na Ochieng Brian, Rafael Ndukwe, Derrick Abdundo, David Kioko, Rick Donald na Omondi Victor.

”Licha ya kupata kibarua kigumu sina shaka kushukuru wenzangu kwa kubeba taji la msimu huu,” mchezaji wa Chrispinus Onyango ambaye huchezea Wazito FC alisema.

Kingstone FC ilituzwa Sh300,000 huku Allin Jua Kali FC ikitia kibindoni Sh100,000. Nayo MASA ilipokeza Sh50,000 kwa kumaliza ya tatu baada ya kudunga Umeme Bees bao 1-0.

Mabingwa hao wanatarajiwa kucheza na mabingwa wa mashindano ya Ndondo Cup ambayo huandaliwa kila mwaka nchini Tanzania sawa na Koth Biro.

Kitengo cha zawadi ya kibinafsi, Francis Omondi wa Borrusia aliibuka mfungaji bora kwa kuitingia mabao matano huku tuzo ya mchezaji anayeimarika (MVP) ikiendea mwenzake Keith Imbali. Evans Mieno wa Umeme Bees alitwaa tuzo ya mchezaji anayelenga kutinga mbali miaka ijayo. Tuzo ya mchezaji aliyeibuka muhimu kwenye mechi hizo iliwaendea Hussein Maina na George Odhiambo wa Kingstone na Allin Jua Kali mtawalia.

Ofisa mkuu wa mashindano hayo Robert ‘Rowbow’ Ocholla na mshirikishi wake Paul ‘Polosa’ Ojenge walishukuru SportPesa kwa kuendelea kudhamini kinyang’anyiro hicho.