• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 7:50 AM
KOTH BIRO: Gattuso ashindwa kubeba Ruaraka katika fainali

KOTH BIRO: Gattuso ashindwa kubeba Ruaraka katika fainali

NA JOHN KIMWERE 

DALLAS Allstars imepambana mwanzo mwisho na kubahatika kutawazwa mabingwa wapya katika shindano la Koth Biro muhula wa 2020-21 ambayo ni makala ya 45. Dallas Allstars iliyotokea eneo la Landmawe ilibeba taji hilo ilipolemea Ruaraka Allstars iliyokuwa ikipigiwa upatu kubeba taji hilo.

Ruaraka Allstars ilishindwa kufanya kweli licha ya kutegemea huduma zake, Collins ‘Gattuso’ Okoth aliyekuwa akipigia Gor Mahia FC ambayo hushiriki Ligi Kuu Kenya.

Vijana wa Dallas wakiongozwa na nahodha, Clinton Olunga walitawazwa mabingwa wa kinyang’anyiro hicho walipofunga Ruaraka Allstars kwa mabao 8-7 kupitia mipigo ya matuta baada kutoka sare tasa katika muda wa kawaida.

Timu hiyo chini ya kocha, Stephen Mbogo huku ikishangaliwa na wafuasi wao waliofurika katika Uwanja wa Umeme Ziwani, Nairobi ilitandaza soka safi na kuonekana kuwalea wapinzani katika kipindi cha kwanza.

Ndani ya kipindi cha pili wachezaji wa timu zote walipata nafasi kadhaa na kushindwa kuzitumia vyema. David Onyango ndiye alipoteza kwa upande wa Ruaraka Allstars na kuchangia kukosa taji hilo.

Wafungaji wa Dallas walikuwa:Dryan Musa, Tyran Owino, Eliakim Muange, Griffins Maloba, Sammy Ben, Michael Amanda, Oscar Masika na Evans Irungu. Nao waliofungia Ruaraka ya Cyril Otieno walikuwa: Kevin Omondi, Collins Ochieng, Manami Lewis, Derrick Owino, Brian Juma, Tyson Otieno na Veron Nanjero.

”Bila shaka tunashukuru sana kuibuka mabingwa wa taji hilo la Koth Biro msimu huu baada ya kulisaka mara mbili bila mafanikio,” nahodha wa Dallas alisema na kuongeza kuwa muhula ujao watakuwa kazini kutetea ubingwa huo.

Mchezaji huyo anasema kwenye mechi za mwaka huu walijitahidi kwa udi na uvumba kukabili wapinzani wao. Dallas iliposhiriki kipute hicho mara ya kwanza ilibanduliwa kwenye mechi za makundi kabla ya kupigwa breki katika robo fainali.

Ruaraka ilishinda Terror Squad kwa mabao 3-1 nayo Dallas Allstars iliandikisha ufanisi wa mabao 5-4 dhidi ya kikosi cha Leads United kupitia mikwaju ya penalti.

Ruaraka Allstars ilijikatia tiketi ya kushiriki mchezo huo baada ya Tyson Otieno kusaidia kufunga Leads United bao 1-0 katika robo fainali. Nayo Githurai United iliumwa mabao 8-7 na Terror Squad kupitia mipigo ya matuta baada ya kutoka nguvu sawa bao 1-1.

Nao wachezaji wa Asec Huruma walizaba Biafra mabao 2-1 huku Dallas ikizoa matokeo sawa na hayo dhidi ya Kajiado Allstars.

Kikosi cha Dallas Allstars kilijumuisha: Clinton Olunga(nahodha), Felix Sambu, Hemstine Smith, Pius Odhiambo, Amos Okoth, Sammy Ben, Michael Amanda, Griffins Maloba, Eliakom Muange na Tyran Owino. Wengine walikuwa Dryan Musa, Eugene Wethuli, Cyrus Mwangi, Ryan Kariuki, Vincent Ajode, Protus Otieno, Kennedy Kimotho, Oscar Masika, Peter Wambua na Evans Irungu.

You can share this post!

Kingi aungama mambo si shwari kwa ODM Pwani

Tyler Onyango afurahia kuchezeshwa na Ancelotti