Kipa ngome ya kuaminika michumani Mount Kenya University FC
NA RICHARD MAOSI
Abraham Wafula ameibukia kuwa miongoni mwa makipa wenye tajriba pana, katika kabumbu ya ligi ya divisheni ya pili FKF ukanda wa kati tawi la Magharibi,vivisasa akiichezea timu wanafunzi ya Mt Kenya University.
Licha ya kutumika kama nguzo muhimu katika kikosi cha Mount Kenya University,pia ni nahodha anayejaza kikosi cha kwanza kinachochiriki michuano ya ligi ,mechi za kirafiki, Inter Estate competition miongoni mwa nyinginezo.
Anasema alianza kucheza mpira yapata 2014 akiwa katika shule ya msingi,mjini Nakuru akishiriki ligi za watoto mitaani,wala hakuwa na ndoto ya kuja kuwa kipa wa kutegemewa.
“Nilipata fursa ya kujiendeleza walimu wa michezo,pamoja na wazazi walipotambua nina kipaji ambacho kingeweza kunifikisha mbali,”akasema Abraham tulipokutana naye katika uwanja wa Nakuru Athletics Club akifanya mazoezi.
Awali alikuwa akicheza kama kiungo wa kati lakini mshambulizi lakini baadae akabadilisha nafasi alipobaini,anamiliki sifa za ugolkipa na angeweza kuzuia mikiki mikali kutoka ndani na nje ya mzunguko wa 18.
Akiwa ni kipa nambari moja anayewajibikia majukumu ya timu ya Mount Kenya,katika mapambano ya mechi nyingi za awali, ameyaruhusu mabao machache tu kuingia langoni pake huku akisimama tisti mbele ya washambulizi.
Msimu wa 2017-2018 alifungwa magoli sita tu katika msimu wote, jambo linalomweka pazuri katika harakati ya kujitengenezea jina kwa vilabu kwenye timu za daraja la juu,zinazohemea huduma zake kama andazi moto.
Abraham aliisaidia timu yake kucharaza Bigot FC,Nakuru All Stars,Ravine Roses na Geothermal Development Cooperation (GDC) ,timu zenye ushindani mkali ligini wa ligi pana ya divisheni ya pili.
“Ninajitahidi kila mara kufanya mazoezi ya kutosha,kwa kujifunza mbinu za makipa wengine ili niweze kufikia kiwango cha kimataifa kwenye ulingo huu wa soka unaohitaji juhudi nyingi,” akasema.
Mchango wake ukiwa ni kulinda ngome na kuisadia walinzi kujipanga karibu na lango.Lakini hata hivyo anawashauri washambulizi wake kufunga magoli mengi,awamu hii wanaposaka nafasi ya kuwa miongoni mwa timu tatu bora ligi inapoelekea ukingoni.
Vilabu kadhaa vya ligi na supa kama vile St Joseph na Green Commandos vimekuwa vikihemea huduma zake lakini Abraham aliamua kusalia katika timu ya Mt Kenya ili kuboresha viwango.
Timu ya Mt Kenya University imekuwa ikitamba mchango wa Abraham akiwa langoni ukiwa ni miongoni mwa sababu kuu.
Wakati mwingi alisaidia timu yake kufanyisha kipa mazoezi lakini hatimaye akaja kumpiku na kuwa chaguo nambari moja kwa timu yake.
Wafula anasema anapania kuisaidia timu yake kushinda mataji,mbali na kuwa kielelezo kwa vijana chipukizi wanaoibukia kutoka mashinani wakiwa na ari ya kuja kusakata mpira kitaaluma.
Wafula anaamini kuwa timu yake inawza kutetemesha timu zenye ushindani mkali katika ligi ya kisasa, endapo wachezaji wenzake watashirikiana kuzalisha matokeo bora.
Aidha anasema cha msingi ni wao kujiamini kama timu na kujituma kila mara wanapoingia uwanjani kuchuana wa sababu kila mchuano huwa na mshindi au mshinde.
Ingawa mchezo wa soka unaendelea kupata changamoto nyingi katika mataifa yanayokuwa,bado vijana wengi hawajakata tamaa kwa sababu kipaji kinalipa.
Wafula anasema kuwa yeye anafuata nyayo za Peter Czech wa Arsenal ambaye ameshinda takriban mataji yote bara uropa na akaastaafu kutoka soka ya kulipwa akiwa amejitengenezea jina ndani na nje .
Mkufunzi Edwin Kwintira wakati akiteua kipa nambari moja alikuwa na mtihani mgumu baada ya makipa wake wote kuonyesha kuwa walikuwa shwari kabisa.
Kwintira anasema alishirikisha waamuzi na wakufunzi wengine kufanya majaribio ya kina, ili kutathmini ubora wa makipa wake wote ndiposa akaangukia Wafula kama chaguo lake la kwanza.
Hata hivyo Wafula anasema ni ndoto yake kuja kucheza soka ya kulipwa katika timu zinazoshiriki kandanda bara ulaya.
Akiamini kuwa uzoefu na weledi utamsaidia kuyatimiza malengo yake anayopania kutimiza katika ulingo wa soka hasa za mbeleni.