Michezo

KIPENGA: Real kumtimua Zidane halafu Mourinho apewe

October 7th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na JOB MOKAYA

TANGU kupewa nafasi nyingine ya kuingoza Real Madrid, Zinedine Zidane ameandikisha msururu wa matokeo mabaya kiasi cha kupoteza imani ya uongozi wa timu.

Hivi sasa, ni suala la lini wala si iwapo atapigwa kalamu.

Atakayepewa mikoba hiyo si mwingine ila ni yule yule, The Special One, Jose Mourinho, aliyeambiwa na rais wa Real Madrid, atulie pembeni kiasi tu, mburukenge Zidane ang’atuliwe ili yeye apawe majukumu.

Mourinho akiwa Manchester United alisumbuliwa sana na kivuli cha Zinedine Zidane wakati matokeo yalipokuwa mabaya. Zidane akiwa tayari kuchukua majukumu ya kuiongoza Manchester United pindi Mourinho afutwapo.

Sasa imekuwa mkuki kwa nguruwe kwa binadamu mchungu. Zidane ndiye anayeandamwa sasa na kivuli cha Jose Mourinho pale Santiago Bernabeu.

Huku Mourinho akisubiria kwa kitambo kidogo, sungosungo ya uga, kudakia tonge atakalolitema Zidane.

Zidane mwenyewe alishinda mataji tisa katika misimu yake mitatu kule Real Madrid; matatu yayo yakiwa kombe la Champions League akiwa ametinga mara tatu mfululizo akiwa kocha wa kwanza kufanya hivo.

Ingawa ni rahisi kuafikia uamuzi kwamba Zizuu kama anavyojulikana Zidane ni kocha mzuri na mwenye haiba ya kufunza timu nyingine kubwa, ukweli ni kwamba Zidane alirithi kikosi imara sana Real Madrid.

Kikosi alichorithi Zidane ndicho kilichokuwa bora zaidi Ulaya kikiwa na wachezaji kama vile Christiano Ronaldo, Karim Benzema, Gareth Bale, Sergio Ramos, Luka Modric, Marcelo, Raphael Varane miongoni mwa wengine.

Ilikuwa rahisi kwa kikosi kama hiki kutamba Ulaya hadi kunyakua kombe la klabu bingwa mara tatu mfululizo, ingawa katika ligi ya Uhispania, La Liga, Zidane alifeli na kumaliza wa tatu.

Endapo matokeo ya Real yataendelea kudorora na kusababisha Zinedine Zidane kupigwa kalamu, basi itakuwa afueni kubwa kwa Mourinho aliyekaa nje kwenye ubaridi kwa muda mrefu baada ya kutimuliwa Old Trafford.

Klabu ya Real Madrid ilimteua tena Zidane kuwa kocha mpya wa klabu hiyo baada ya kumpiga kalamu Santiago Solari ambapo wengi walidhani kwamba Mourinho angepewa kazi hiyo.

Jose Mourinho naye alikuwa amepigiwa upatu kupewa tena hatamu za kuiongoza Real Madrid na tangazo la yeye kepewa mikoba ya kazi lilitarajiwa kutolewa wakati wowote huku vyombo vingi vya habari duniani vikisoma habari hizo.

Kutangazwa kwa Zidane kuliwashangaza wengi, siyo kuhusu uwezo wake, bali namna alivyombwaga The Special One katika nafasi hii.

Mchuano huu ambao ulionekana kuelemea upande mmoja wa Mourinho ukashindwa kwa urahisi na Zizuu.

Tayari wale waliokuwa na shaka kuhusu uwezo wa Zidane, huenda shaka yao imeanza kudhihirika kwani Real Madrid imeshindwa kutamba kwenye mechi za kirafiki za kimataifa.

Licha ya kupata huduma za Hazard, bado huyo Hazard hafanyi lolote la maana na mchezaji mwingine mwenye uwezo wa Ronaldo, Lionel Messi, Neymar au Kylian Mbappe atahitajika katika safu ya ufungaji naye Paul Pogba ahitajike pale katikati kumwokoa Zidane.

Hayo yakijiri, tayari Mourinho ameanza kutafuta mbinu ya kumwondoa hasidi wake Ramos na Marcelo kwenye kikosi cha Real Madrid na kuleta wachezaji wengine watakaounga mkono mbinu zake.

Tayari Mourinho alizuia kusajiliwa kwa hasidi wake Pogba na Real Madrid.