Michezo

Kisumu kuandaa Elgon Cup 2019, ni mara ya kwanza Kenya inaandaa kombe hili nje ya Nairobi

March 29th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

MJI wa Kisumu umeteuliwa kuandaa mechi ya nyumbani ya Kenya ya raga ya kimataifa ya wachezaji 15 kila upande ya Elgon Cup dhidi ya Uganda mwaka 2019.

Hii ni mara ya kwanza kabisa mkondo wa kombe hili unaenda nje ya Nairobi.

Taarifa kutoka Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) inasema kwamba Kisumu ilituma ombi kuwa mwenyeji wa kombe hili mwaka 2018 na kukubaliwa na shirikisho hilo kama mpango wake wa kusambaza mechi za kimataifa. “Kuandaa mchuano huu mjini Kisumu ni mojawapo ya mpango wa KRU kusambaza mechi za kimataifa. Klabu zingine pia zinashawishiwa kuomba mashindano mengine ya kimataifa kwa sababu itachangia pakubwa katika kuimarisha vifaa vyao pamoja na kukuza mchezo wa raga. Tayari klabu zimeonyesha zina uwezo wa kuvutia umati wa mashabiki na tumeshuhudia hivyo mjini Kisumu wakati wa duru ya kitaifa ya raga ya wachezaji saba kila upande ya Dala Sevens,” alisema Naibu Mwenyekiti wa KRU, Thomas Opiyo.

Timu ya taifa ya raga ya wachezaji 15 kila upande ya Kenya almaarufu Simbas inatarajiwa kuanza matayarisho baada ya Ligi Kuu (Kenya Cup) kutamatika Mei 11.

Gavana afurahia

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mji wa Kisumu kuwa mwenyeji wa Elgon Cup mwaka 2019 hapo Machi 28, Gavana wa Kisumu, Profesa Anyang’ Nyong’o alisema, “Hii ni mara ya pili tunazindua shindano la raga katika kaunti ya Kisumu na tunatumai haitakuwa mara ya mwisho. Lengo letu ni kusaidia michezo kikamilifu katika kaunti hii ili Kenya iweze kupata sehemu ya kukuza wanariadha na wanaspoti wake kutoka kaunti hii. Ugatuzi unamaanisha kwamba kila mtu humu nchini ajihisi hajaachwa nje katika sehemu zote za maisha.”

“Nafurahia sana Elgon Cup kuja Kisumu mwezi Juni mwaka 2019. Tumekuwa tukilenga kukuza nafasi yetu mjini Kisumu kama mji wa mashindano makubwa na ninakaribisha timu ya Uganda pamoja na mashabiki wote kutoka eneo hili,” aliongeza Achie Alai, Waziri wa Utalii na Michezo wa kaunti ya Kisumu.

Kenya itakuwa ikitetea taji ililoshinda mwaka 2018 kwa kuchabanga Uganda 34-16 jijini Kampala mwezi Mei na kulemea majirani hao wake tena 38-22 Julai.