Michezo

Kivumbi Atletico Madrid wakialika Liverpool leo Jumanne

February 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

MADRID, UHISPANIA

ATLETICO Madrid watakuwa leo Jumanne wenyeji wa Liverpool katika mkondo wa kwanza wa hatua ya 16-bora ya kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) uwanjani Wanda Metropolitano, Uhispania.

Ni patashika ambayo kocha Diego Simeone wa Atletico ameonya kwamba itatawaliwa na hisia kali kwa kuwa itawapa masogora wake jukwaa la kupima ubabe wao dhidi ya pengine kikosi bora zaidi duniani.

Katika kivumbi kingine Jumanne, Borussia Dortmund watawakaribisha Paris Saint-Germain (PSG) ugani Signal Iduna Park, Ujerumani.

Itakuwa ni mara ya tatu kwa miamba hawa kukutana tangu waambulie sare tasa kwenye mechi za mikondo miwili ya UEFA katika msimu wa 2010-11.

Dortmund waliobanduliwa na Tottenham Hotspur katika hatua hii ya 16-bora msimu jana, walikamilisha kampeni zao za Kundi F muhula huu nyuma ya Barcelona watakaovaana na Napoli wiki ijayo.

Licha ya kwamba huu ni msimu wao wa 14 katika gozi la UEFA, wanajivunia kutinga fainali mara moja (2013) na kuonja robo-fainali mnamo 2016-17.

Kufikia sasa, Atletico wanashikilia nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) kwa alama 40 sawa na Sevilla. Ingawa hivyo, ndicho kikosi cha tatu bora zaidi jijini Madrid baada ya viongozi Real na Getafe.

Kwa upande wao, Liverpool wanajivunia msimu wa kuridhisha sana ambapo kwa sasa wanahitaji alama 15 pekee kutokana na mechi 12 zilizosalia ili kutawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30.

Pengo la alama 25 linatamalaki kati ya Liverpool na mabingwa watetezi Manchester City ambao kesho watawaalika West Ham United kwa kivumbi cha EPL ugani Etihad kabla ya kunoa kucha za kuwakwaruza Real ugani Santiago Bernabeu wiki ijayo katika UEFA.

Ingawa Atletico wanapigiwa upatu wa kutikisa uthabiti wa Liverpool ambao ni mabingwa watetezi wa UEFA, huenda kibarua hicho cha leo kikawa kigumu hasa ikizingatiwa wingi wa visa vya majeraha kambini mwa kocha Simeone.

Mbali na Kieran Trippier anayeuguza jeraha la paja, nyota Joao Felix pia atakosa kuwasakatia Atletico kutokana na tatizo la goti. Chipukizi huyo mwenye umri wa miaka 20 alisajiliwa kutoka Benfica kwa kima cha Sh16 bilioni mwishoni mwa msimu uliopita.

Kutokuwepo kwa Diego Costa atakayesalia mkekani kwa wiki tatu, kutamweka Simeone katika ulazima wa kumtegemea pakubwa fowadi wa zamani wa Chelsea, Alvaro Morata ambaye amepachika wavuni zaidi ya robo moja ya mabao yote yanayojivuniwa na Atletico kwa sasa katika mapambano yote msimu huu.

Kinyume na wenyeji wao, Liverpool watakosa huduma za beki Nathaniel Clyne pekee.