KLABU ZAVUNA: Jua ni timu zipi zilisajili wachezaji mahiri
Na AFP
PARIS, UFARANSA
KLABU za PSG, Juventus na Atletico Madrid ndizo zilifanikisha usajili wa wachezaji mahiri huku Manchester United, Real Madrid na Barcelona zikiangukia pua na kukosa kufanikisha uhamisho wa wachezaji nyota waliolenga kujumuisha kwenye vikosi vyao msimu huu.
PSG ya Ufaransa ilionekana kifua mbele siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha hilo la usajili wa wanasoka baada ya kutwaa huduma za mshambulizi Mauro Icardi na mnyakaji Keylor Navas kutoka Inter Milan na Real Madrid mtawalia.
Kusajiliwa kwa Navas kwa mkataba wa miaka minne kulimwezesha aliyekuwa nyani wa PSG Alphonse Areola pia kujiunga na Inter Milan kwa mkopo.
Navas ambaye amechezea Costa Rica mara 86 alipoteza nafasi yake langoni kwa Thibaut Courtois ambaye alisajiliwa na mibabe hao kutoka Chelsea mwanzo wa msimu wa 2018/19.
Hata hivyo, atalazimika kuwania nafasi ya kuanza mechi kambini mwa PSG pamoja na kipa Sergio Rico ambaye alisajiliwa kwa mkopo na kocha Thomas Tuchel kutoka Sevilla ya Uhispania Jumapili iliyopita.
Icardi, 26 ambaye mwishoni mwa msimu jana alikosana na usimamizi wa Inter Milan, naye alisajiliwa kwa mkopo wa miaka miwili ila PSG wataruhusiwa kutwaa huduma zake kabisa iwapo watalipa Sh7 bilioni kabla ya kandarasi hiyo kutamatika.
Icardi alikuwa amehudumu kambini Nerazzurri kwa muda wa miaka sita na kuwafungia mabao 124 baada ya kucheza mara 219.
Nchini Uingereza juhudi za kiungo Paul Pogba kujiunga na Real Madrid ziligonga mwamba baada ya kocha Zinedine Zidane kukosa kufaulisha uhamisho huo ambao ulisubiriwa kwa hamu na ghamu na mashabiki ugani Santiago Bernabeu.
Uongozi wa Real Madrid ulikosa kutimiza nia ya Zidane ya kumtaka kuwatimua Gareth Bale na James Rodriguez kisha anunue Pogba kuchukua nafasi ya wawili hao.
Hata hivyo, inadaiwa Rais wa Real Madrid Florentino Perez alikataa kuidhinisha uhamisho wa nyota hao wawili ikizingatiwa kwamba winga Marco Asensio bado ana jeraha ambalo litamweka nje kwa muda mrefu msimu huu.
Zidane sasa atalazimika kutegemea huduma za aliyekuwa kiungo wa Chelsea Eden Hazard ambaye alisajiliwa mapema kuvumisha timu hiyo. Wachezaji wengine waliosajiliwa na Zinedine Zidane ni Eder Militao, Rodrygo, Luka Jovic na Ferland Mendy.
Baada ya kuwapoteza Diego Godin, Antoine Griezmann, Rodri, Lucas Hernandez, Juanfran na Filipe Luis, Atletico Madrid pia waliimarisha kikosi chao na kwa kumsajili Kieran Trippier, Marcos Llorente na Joao Felix. Sajili hawa wapya tayari wameanza kuwavumisha vijana wa Diego Simeon baada ya kuvuna ushindi kwenye mechi tatu za mwanzo za La Liga.
Juventus ya Italia pia walionekana kuvuna vizuri kwenye usajili baada ya kutwaa huduma za Matthijs de Ligt kutoka Ajax, Adrien Rabiot(PSG) na Aaron Ramsey kutoka Arsenal.
Hata hivyo, juhudi za Juve kumlazimisha mshambulizi Paulo Dybala kuelekea Manchester United kisha warejeshe Pogba ambaye aliwasakatia kabla ya kuyoyomea Red Devils ziligonga mwamba.
Kocha wa Juventus Maurizio Sarri sasa atategemea huduma za mafowadi Gonzalo Higuain, Mario Mandzukic, na Cristiano Ronaldo msimu mzima.
Barcelona pia waliangukia pua kwenye usajili huo baada ya nia yao ya kumrejesha Neymar Jnr ugani Camp Nou kugonga mwamba.
Hii ni baada ya wachezaji Ousmane Dembele na Ivan Rakitic kukataa kuhamia PSG ili kupisha Neymar kurejea kuunga safu kali ya mashambulizi pamoja na Lionel Messi na Luis Suarez.