Klabu zilizopandishwa zakosa ustadi unaohitajika ligi ya daraja la pili
Na CECIL ODONGO
MICHUANO ya ligi ya daraja la pili iliingia raundi ya sita wikendi iliyopita huku mechi sita zikisakatwa na timu mbalimbali zilizoshiriki mechi hizo zikisajili matokeo ya mseto.
Klabu ya Ushuru FC walioshushwa daraja kutoka ligi kuu ya KPL mwaka 2017 walipata ushindi mwembamba wa 1-0 dhidi ya Green Commandoes ya Kakamega.
Kwa sasa wanaushuru hao wanaonolewa na Kocha Ken Kenyatta wanashikilia nafasi ya kumi kwenye msimamo wa jedwali ya ligi hiyo.
Hata hivyo klabu nyingine zilizokuwa zikishiriki ligi kuu miaka ya nyuma zilisajili matokeo yasiyoridhisha hii ikiwa ishara tosha kuwa ligi hiyo inashuhudia ushindani mkali.
Klabu ya Nakuru All stars iliadhibiwa vikali na Bidco FC kwa mabao 5-0,Western Stima ambao pia waliteremshwa ngazi kutoka KPL mwaka jana wakaenda sare ya 2-2 na limbukeni St Joseph youth Uwanjani Moi Kisumu.
Aidha Nairobi CIty stars hawakusazwa walipokalifishwa 1-0 na Isbania FC kule Awendo green Stadium.
Kwenye matokeo mengine klabu ya FC Talanta walitoka sare tasa dhidi ya wapinzani wao Kisumu All Stars nao Modern Coast Rangers wakaagana 1-1 na Coast Stima kwenye debi ya Pwani iliyosakatwa uwanjani Mbaraki kaunti ya Mombasa.
Hadi sasa Kibera Black Stars wanaongoza msimamo wa jedwali la ligi hiyo kwa alama 13 baada ya kutopoteza mechi yoyote.Klabu za Bidco,Western stima, Isbania FC na Kisumu All Stars zinafunga orodha ya tano bora.
Klabu za Green commandoes,Administration Police na Nakuru All Stars zinafunga orodha za klabu tatu ambazo zinaning’inia padogo kwenye eneo hatari ya kushushwa ngazi.
Mtanange kati ya timu nyinginezo hazikuchezwa na ratiba kupangwa upya kutokana na timu hizo kutumia uwanja moja na wenzao wanaoshiriki ligi kuu ya KPL.