Klopp awapiku Lampard, Rodgers na Wilder kwenye tuzo za kocha bora wa mwaka katika EPL
Na CHRIS ADUNGO
KOCHA Jurgen Klopp wa Liverpool ametawazwa Kocha Bora wa Mwaka katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu wa 2019-20.
Mkufunzi huyo mwenye umri wa miaka 53 aliwaongoza Liverpool kunyanyua ubingwa wa EPL kwa mara ya kwanza muhula huu baada ya kusubiri kwa kipindi cha miaka 30.
Chini ya kocha huyo mzawa wa Ujerumani, Liverpool walijizolea jumla ya alama 99 baada ya kushinda mechi 32 kati ya 38.
Ufanisi huo uliwawezesha kukamilisha kampeni hizo kwa pointi 18 zaidi kuliko Manchester City walioridhika na nafasi ya pili.
Klopp aliwapiga kumbo Frank Lampard wa Chelsea, Brendan Rodgers wa Leicester City na Chris Wilder wa Sheffield United waliokuwa washindani wake wengine katika juhudi za kuwania tuzo hiyo.
Klopp anatuzwa siku mbili baada ya beki Trent Alexander-Arnold wa Liverpool, 21, kutawazwa Chipukizi Bora wa Mwaka.
Mwezi jana, Klopp alitawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka katika tuzo za Chama cha Wakufunzi wa Soka ya Uingereza (LMA).
Emma Hayes wa Chelsea alitawazwa Kocha Bora wa Mwaka kwa upande wa wanawake baada ya kuwaongoza vipusa wake kutia kapuni ubingwa wa Ligi Kuu ya FA Women’s Super msimu huu.
Mkufunzi Marcelo Bielsa wa Leeds United alitwaa tuzo ya Kocha Bora wa Mwaka katika Ligi ya Daraja la Kwanza (Championship) baada ya kuongoza kikosi chake kurejea katika soka ya EPL baada ya kuwa nje kwa miaka 16.
“Ni fahari tele kutawazwa Kocha Bora na kupokezwa tuzo hii ambayo kwa hakika imechangiwa na familia nzima ya Liverpool,” akasema Klopp ambaye aliandamana kwa hafla hiyo na makocha wote wasaidizi wa Liverpool – Pep Lijnders, Peter Krawietz, John Achterberg, Vitor Matos na Jack Robinson.
Bill Shankly, Bob Paisley, Joe Fagan, Sir Kenny Dalglish na Brendan Rodgers ndio wakufunzi wengine wa hivi karibuni kutwaa taji la Kocha Bora wa Mwaka kabla ya Klopp.