Kocha Frank Lampard aeleza jinsi ujuzi unavyomfaidi
Na MASHIRIKA
LONDON, Uingereza
KOCHA Frank Lampard wa Chelsea amefichua jinsi ujuzi wake wa muda mrefu unavyomsaidia katika majukumu yake ya kuiongoza klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) pale Stamford Bridge.
Katika mahojiano ya kibinafsi, kiungo huyo mstaafu amesema ujuzi wake kama mchezaji na pia naibu nahodha wa klabu hiyo kwa miaka mingi umemsaidia zaidi katika kutimiza malengo yake kama kocha, hasa unapofika wakati wa kutoa maamuzi magumu kila wakati.
“Ukiwa kocha wa timu lazima ukabiliwe na hali ngumu, hasa inapofika wakati wa kuunda kikosi cha kwanza. Lazima uchukuwe msimamo na uwe tayari kujitetea,” alisema.
“Niliizoea hali hii nikiwa mchezaji kutoka kwa makocha mbalimbali, hata wale walionipuuza ama kunipa namba ambayo sio yangu. Binafsi nilijifunza mengi kutoka kwa John Terry aliyekuwa nahodha mkuu ambaye sasa ni naibu wa kocha wa klabu ya Aston Villa,” alisema.
Tangu achukue usukani, Lampard ameandikisha matokeo mengi mazuri, ingwa kumekuwa pia na mengine ya kuchanganya kwa kikosi chake ambacho kinashikilia nafasi ya nne jedwalini tangu ligi isimamishwe zaidi ya miezi miwili iliyopita kutokana na janga na corona.