Michezo

Kocha Genot Rohr awataka vijana wake kuepuka makosa madogomadogo

July 10th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA na CECIL ODONGO

MKUFUNZI wa timu ya taifa ya Nigeria, Genot Rohr, amewataka wachezaji wake kuyaepuka makosa madogomadogo wanapokutana na Afrika Kusini Jumatano usiku katika mechi ya robo fainali ya kipute cha Mataifa Bingwa Barani Afrika (AFCON).

Super Eagles waliizawidi Madagascar bao rahisi kwenye kichapo walicholishwa katika mechi ya mwisho ya kundi lao la B wakati pasi mbovu ya John Ogu kwa mchezaji mwenzake Leom Balogun ilichangia bao la kwanza la vijana wa kisiwani.

Ulegevu wa safu ya ulinzi ya Super Eagles ulidhihirika zaidi kwenye ushindi wa 3-2 dhidi ya Cameroon pale mlinzi Ola Aina alichelewa kutoa mpira kwenye eneo la hatari na kumpa mshambulizi Njie Clinton nafasi ya kutinga bao la pili.

Ingawa Super Eagles ilishinda Cameroon, Rohr amewataka vijana wake kuwa makini kwa kuwa kikosi cha Afrika Kusini kinajivunia wachezaji wenye kasi ya juu waliojipanga vyema katika kila safu.

“Kila kitu kinawezekana kwenye kipute hiki cha Afcon na kosa lolote linaweza kuzidishia wachezaji wa kikosi chochote presha uwanjani. Lazima tujihadhari, tucheze kwa kujituma na tuepuke makosa madogo ili tusifungwe mabao rahisi jinsi ilivyokuwa katika mechi za awali dhidi ya Madagascar na Afrika Kusini,” akasema Rohr.

Akaongeza: “Inasikitisha kwamba makosa yaliyotuponza kwenye mechi mbili za awali yanatokana na makosa ya wachezaji binafsi na hayahusiani na mfumo wetu wa kusakata kabumbu. Natumai katika mechi dhidi ya Afrika Kusini hali itakuwa toafuti hasa ikizingatiwa tunalenga kufuzu nusu fainali.”

Mechi kati ya Bafana Bafana na Nigeria itaanza saa nne kamili usiku saa za Afrika Mashariki na ni mojawapo ya mechi ambayo imetajwa kuwa itakuwa na ushindani mkali.