Kocha Martinez arefusha mkataba Ubelgiji
CHRIS ADUNGO na MASHIRIKA
KOCHA mkuu wa timu ya taifa ya Ubelgiji, Roberto Martinez, 46, amesema analenga kuacha “kumbukumbu nzuri” katika ulingo wa soka baada ya kurefusha mkataba wake kambini mwa kikosi hicho hadi mwishoni mwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar.
Kocha huyo mzawa wa Uhispania alipokezwa mikoba ya Ubelgiji mnamo 2016 na kandarasi yake ilikuwa itamatike rasmi mwishoni mwa fainali za Euro 2020 ambazo kwa sasa zimeahirishwa hadi mwaka 2021 kutokana na janga la corona.
“Nina fahari kurefusha muda wa kuhudumu kwangu kambini mwa Ubelgiji. Nahisi kwamba ningali na fursa ya kufanikisha kampeni za Ubelgiji katika mapambano mengi ya haiba kubwa na kuacha kumbukumbu nzuri za kudumu ndani ya kikosi hicho,” akasema mkufunzi huyo wa zamani wa Everton, Swansea City, na Wigan Athletic.
Chini ya Martinez, Ubelgiji waliambulia nafasi ya tatu kwenye fainali za Kombe la Dunia zilizoandaliwa nchini Urusi mnamo 2018.
Kufikia sasa, Ubelgiji wanaselelea kileleni mwa orodha ya viwango bora vya Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) na wanajivunia kusajili ushindi katika mechi zote 10 za kufuzu kwa fainali za Euro 2020.
Wanapigiwa upatu wa kutawala Kundi B linalowajumuisha pia Denmark, Finland na Urusi na pengine hatimaye kunyanyua ufalme wa fainali zijazo za Euro.
“Kubwa zaidi katika maazimio yangu kwa sasa ni kuwavunia Ubelgiji ubingwa wa Euro na Kombe la Dunia katika kipindi kijacho cha mkataba wangu mpya,” akasema Martinez aliyewahi pia kuchezea kikosi cha Real Zaragoza cha Uhispania wakati wa usogora wake.
Ubelgiji ni miongoni mwa timu zinazojivunia huduma za wanasoka matata zaidi duniani kwa sasa wakiwemo Eden Hazard (Real Madrid), Romelu Lukaku (Inter Milan), Kevin de Bruyne (Manchester City), Thibaut Courtois (Real), Vincent Kompany (Anderlecht), Christian Benteke (Crystal Palace) na Divock Origi (Liverpool).