Michezo

Kocha Maurizio Sarri atastahimili mawimbi ya misukosuko Chelsea?

February 21st, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA na GEOFFREY ANENE
MAURIZIO Sarri atapigwa teke na Chelsea ikipoteza mojawapo ya mechi zake tatu zijazo dhidi ya Malmo (Ligi ya Uropa), Manchester City (League Cup) na Tottenham Hotspur (Ligi Kuu) uwanjani Stamford Bridge, tetesi zinasema.
Chelsea itaalika Malmo kutoka Uswidi mnamo Februari 21 ilimane na City katika fainali ya League Cup hapo Februari 24 na kupepetana na Spurs mnamo Februari 27.
Ripoti nchini Uingereza zinasema Mwitaliano Sarri amepoteza uungwaji mkono na viongozi wa Chelsea, ambayo mmiliki wake Roman Abramovich anafahamika kukosa utulivu na makocha wasioletea klabu hii matokeo mazuri.
Sarri, ambaye alijiunga na Chelsea mnamo Julai 24, 2018, saa 24 baada ya Mwitaliano mwenzake Antonio Conte kufurushwa, anakabiliwa na siku saba muhimu zaidi kipindi hiki chake cha kwanza nchini Uingereza.
Kocha Maurizio Sarri wa klabu ya Chelsea. Picha/ AFP
Baada ya kuanza maisha yake ya Chelsea kwa kutoshindwa mechi 18 katika mashindano yote kutoka Agosti 11 hadi Novemba 11 mwaka 2018, Sarri ameshuhudia vijana wake wakipoteza mara nane katika mechi 23 zilizopita. Kinachomweka pabaya kuangukiwa na shoka ni msururu wa matokeo duni Chelsea iliandikisha ligini ilipokung’utwa na Arsenal 2-0, Bournemouth 4-0 na Manchester City 6-0 na itaingia mechi ya leo ikiuguza kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Manchester United kwenye Kombe la FA.
Sarri alinukuliwa na vyombo vya habari nchini Uingereza akisema, “Tunahitaji kushinda mechi tatu ama nne zinazofuata ndiposa niponee. Hiyo ndiyo suluhu ya pekee.” Chelsea ilishinda Malmo 2-1 katika mechi ya mkondo wa kwanza mnamo Februari 14. Iliongoza 2-0 kupitia mabao ya Ross Barkley na Olivier Giroud yaliyopatikana dakika za 30 na 58 kabla ya Anders Christiansen kupachika bao la kufutia machozi dakika ya 80.