Michezo

Kocha Oktay akanusha tetesi za kutoroka Gor Mahia

July 31st, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CECIL ODONGO

KOCHA wa Gor Mahia Hassan Oktay ambaye aliondoka nchini jana kuelekea Uturuki, amefutilia mbali tetesi kwamba ameagana na timu hiyo.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo, Oktay alifafanua kwamba hajaacha kazi ya kuwanoa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu(KPL) ila aliomba ruhusa ya kurejea kwao kuyashughulikia masuala ya kibinafsi ya kifamilia kisha arejee Jumapili.

“Nakuhakikishia kwamba sijaondoka Gor Mahia. Nilizungumza na mwenyekiti Ambrose Rachier na kumwomba anipe siku tano niende nyumbani kushughulikia masuala ya kidharura ya familia. Nitarudi Jumapili na taarifa zinazodai nimejiondoa ni uongo,” akasema Oktay.

Akaongeza: “Nimeifunza Gor tangu msimu uliopita, kuwashindia taji la ligi na pia kuwafikisha kwenye robo fainali ya mechi ya CAF ambayo hatukushinda kutokana na matatizo kati ya wachezaji na uongozi. Japo nilikuwa nimeazimia kuagana nao kabla ya msimu kuanza, nilikutana na Rachier juzi na hakuna wakati nimetangaza nimesitisha kuwapokeza huduma zangu.”

Mkufunzi huyo pia alipuuza habari kwamba mshambulizi mkongwe Dennis ‘The Menace’ Oliech ameteuliwa kuhudumu kwenye benchi ya kiufundi ili kusaidiana na Naibu Kocha Patrick Odhiambo atakapokuwa Uturuki.

“Sina habari kuhusu Oliech kuteuliwa kwenye usimamizi. Kwa sasa ni uongo na iwapo zitatokea kuwa ukweli basi nitatafakari upya kwa sababu lazima nishauriwe kama kocha kabla mabadiliko yoyote kutekelezwa timuni. Odhiambo atasimamia timu hadi nirejee na tumekuwa na uhusiano imara naye tangu ajiunge na timu kutoka SoNy Sugar,” akasema.

Afisa Mkuu Mtendaji, Omondi Aduda alichemkia taarifa hizo, akisema kusafiri kwa Oktay si dalili kwamba ametoroka K’Ogalo.

“Hassan ni mtu mwadilifu na hajawahi kutuficha chochote. Jinsi alivyokueleza, alimwambia mwenyekiti kwamba ana mambo ya dharura nyumbani yanayohusu familia yake na ameenda kuyatatua.”