Michezo

K’Ogalo kuwakosa Oliech, Batambuze dhidi ya Zamalek

March 7th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

GOR Mahia watalazimika kukosa huduma za wachezaji Dennis Oliech na Shafik Batambuze katika mchuano wa mkondo wa pili wa Kombe la Mashirikisho (CAF) dhidi ya Zamalek SC ya Misri mwishoni mwa wiki hii.

Fowadi Oliech anauguza jeraha la mguu huku Batambuze akitumikia marufuku. Beki huyu mzawa wa Uganda alikuwa miongoni mwa masogora watano wa Gor Mahia ambao walionyeshwa kadi za manjano wakati wa mechi iliyowakutanisha na NA Hussein Dey nchini Algeria wikendi jana.

Kwa mujibu wa mtandao wa Goal.com uliomhoji kocha Hassan Oktay ambaye kwa sasa anakinolea kikosi chake nchini Misri, jeraha la Oliech si baya sana.

Dennis Oliech. Picha/ Maktaba

“Japo jeraha lenyewe ni dogo, Oliech hatakuwa sehemu ya kikosi cha Gor Mahia dhidi ya Zamalek. Batambuze aliyekuwa tegemeo zaidi dhidi ya Dey alionyeshwa kadi nyingine ya manjano itakayomweka nje,” akasema Oktay.

Oliech alikuwa miongoni mwa wafungaji katika ushindi wa 4-2 uliosajiliwa na Gor Mahia dhidi ya Zamalek katika mchuano wa mkondo wa kwanza uliowakutanisha uwanjani MISC Kasarani, Nairobi mnamo Februari 3, 2019.

Ufanisi huo ulichangia kudumu kwa Gor Mahia kileleni mwa Kundi D kwa muda hadi walipodenguliwa na Dey wikendi jana baada ya kuchabangwa 1-0 katika uwanja wa Stade 5 Juillet 1962 jijini Algiers, Algeria.

Mechi itakayowakutanisha Gor Mahia na Zamalek jijini Alexandria mnamo Jumapili itakuwa ya kufa kupona kwa vikosi hivyo vinavyopania kuweka hai matumaini ya kusonga mbele katika kipute cha CAF msimu huu.

Mbali na matokeo ya Gor Mahia dhidi ya Dey, ushindi wa 1-0 uliosajiliwa na Zamalek dhidi ya Atletico Petro de Luanda nchini Angola wikendi iliyopita, pia uliacha Kundi D likiwa wazi.

Petro watakuwa wenyeji wa Dey mwishoni mwa wiki hii.

Kinyang’anyiro

Zikisalia mechi mbili pekee kwa mapambano ya makundi kukamilika rasmi, vikosi vyote vya Kundi D vingali na uwezo wa kufuzu kwa hatua ya robo-fainali.

Baada ya kumenyana na Zamalek, Gor Mahia watakuwa wenyeji wa Petro de Luanda ambao waliwazamisha kwa mabao 2-1 katika mkondo wa kwanza nchini Angola mnamo Februari 13.

Gor Mahia ambao wanajivunia pointi sita wanashikilia nafasi ya pili kwa alama sita, moja zaidi kuliko Zamalek.

Vikosi viwili vitakavyotawala kilele cha kila kundi vitafuzu kwa raundi ijayo.