Michezo

Kwa sasa ni mlima kwa Spurs kutinga Nne Bora – Hugo Lloris

March 11th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CECIL ODONGO

NAHODHA wa Tottenham Hot Spurs Hugo Lloris ameeleza wasiwasi wake kuhusu kudorora kwa fomu ya timu hiyo, hali inayoweka hatarini nafasi yao ya kutinga nne bora kwenye Ligi ya Kuu ya Uingereza(EPL).

Mnyakaji huyo wa timu ya taifa ya Ufaransa Les Blues  hata hivyo amesema pumziko fupi na kambi ya wiki mbili watakayokita nchini Uhispania kabla ya mechi ya Machi 31 dhidi ya Liverpool itawasaidia kurejelea fomu yao ya awali ya kutisha.

Spurs inayofundishwa na kocha Mauricio Pochettino ina pengo la alama nne kati yake na nambari sita Chelsea huku ikifuatwa kwa karibu na Arsenal na Manchester United katika nafasi ya nne na tano mtawalia.

Timu hiyo kutoka Kaskazini mwa mji wa London iliendeleza msururu wa matokeo mabaya Jumamosi Machi 9 ilipochapwa 2-1 na Southhampton uwanjani St Marys.

Ingawa hivyo, nyani huyo amesema kwamba ni mapema sana kubaini timu zitakazochukua nafasi za kushiriki Ligi ya Klabu Bingwa Barani Uropa(UEFA) msimu ujao wa 2019/20 kutokana na ushindani mkali unaoendelea kushuhudiwa kati ya Chelsea, Arsenal, Tottenham Hot Spurs na Manchester United.

“Ni mapema sana kuzungumzia UEFA. Bado tupo kwenye kinyángányiro  ingawa lazima tubadilishe mkondo wa mambo ili tuwe na matumaini ya kufuzu,’’

“Fomu yetu ya sasa katika EPL inasikitisha sana kwasababu hatujasajili ushindi wowote kwenye mechi nne zilizopita. Ni vibaya sana kupoteza mechi kwasababu inatuelekeza katika kupoteza dira na kupitwa na wapinzani jedwalini,” akasema Lloris.

Mlinzi Ben Davies akiunga mkono mtazamo wa nahodha wake hata hivyo amepuuza taarifa kwamba wamekuwa wakipepetwa na wapinzani kutokana na uchovu unaowakabili kwa kuwajibikia mechi nyingi kwa muda mfupi.

Spurs ilicheza mechi tano katika kipindi cha wiki mbili. Ilienda sare ya 1-1 dhidi ya Arsenal kwenye debi ya London Kaskazini na kushinda 1-0 mechi Uefa dhidi ya Borussia Dortmund huku wakipigwa katika mechi nyingine tatu kwenye EPL.