• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
Leeds United yapanda ngazi kushiriki EPL baada ya kukaa kwa baridi miaka 16

Leeds United yapanda ngazi kushiriki EPL baada ya kukaa kwa baridi miaka 16

Na CHRIS ADUNGO

KLABU ya Leeds United imepandishwa ngazi kushiriki Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu ujao wa 2020-21 baada ya kukaa nje kwa kipindi cha miaka 16.

Nafasi yao katika EPL ambayo ni ligi maarufu zaidi duniani ilithibitishwa kwa kichapo cha 2-1 ambacho West Bromwich Albion walipokezwa na Huddersfield Town mnamo Julai 17, 2020.

Leeds wanaselelea kileleni mwa jedwali la Championship kwa alama 87, tano kuliko West Brom ambao wanawazidi nambari tatu Brentford kwa pointi moja pekee. Zikisalia mechi mbili pekee kabla ya kampeni za msimu huu kutamatika rasmi, Fulham wanafunga orodha ya nne-bora kwa alama 77.

Leeds kwa sasa watatawazwa mabingwa wa Ligi ya Daraja la Kwanza katika soka ya Uingereza (Championship) iwapo Brentford watashindwa kuwaangusha Stoke City mnamo Julai 18 au iwapo watajizolea hata alama moja dhidi ya Derby County mnamo Julai 19, 2020.

Kocha mzawa wa Argentina, Marcelo Bielsa, amewaongoza Leeds United walio na makao makuu jijini Yorkshire kufuzu kwa kivumbi cha EPL msimu huu ambao ni wake wa pili kambini mwa kikosi hicho kilichoambulia nafasi ya tatu katika Championship mnamo 2018-19

Chini ya Bielsa, Leeds walianika ukubwa wa matamanio ya kunogesha kivumbi cha EPL muhula ujao tangu mwanzoni mwa msimu huu na hawajawahi kujipata nje ya mduara wa vikosi viwili vya kwanza kileleni mwa jedwali tangu Novemba 2019.

Walikuwa pua na mdomo kufuzu kwa kipute cha EPL msimu huu wa 2019-20 mwaka jana ila wakapoteza mechi mbili mfululizo za mwisho wa muhula dhidi ya Wigan na Brentford na hivyo kusalia katika nafasi ya tatu nyuma ya Sheffield United, Norwich City na Aston Villa waliokwea ngazi.

Isitoshe, walipepetwa na Derby County 4-3 katika mechi ya kutafuta mbabe wa jiji la Yorkshire, Uingereza msimu uliopita.

Ingawa kichapo hicho kilitarajiwa kumpa Bielsa kila sababu ya kuagana na Leeds hasa ikizingatiwa ukubwa wa uwezo wa kikosi alichokisuka, kocha huyo alipania kusalia kambini mwa waajiri wake na akatiwa hamasa zaidi na mashabiki ambao kwa sasa wamevuna matunda la jasho lao.

Imekuwa subira ya kipindi kirefu kwa mashabiki wa Leeds walioshuhudia kikosi chao kikitamba katika soka ya Uingereza na bara Ulaya katika miaka ya awali kiasi cha kutinga nusu-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 2001.

Shabiki akiwa amevalia maski ya Leeds United nje ya uwanja wa Elland Road Julai 17, 2020, akisherehekea ufanisi wa timu hiyo kufuzu ligi kuu ya EPL baada ya kuwa nje miaka 16. Picha/ AFP

Leeds walikuwa katika hali mbaya zaidi ya kifedha waliposhuka ngazi hadi Ligi ya Championship mnamo 2004.

Hata hivyo, kocha Kevin Blackwell ambaye ni miongoni mwa wakufunzi 15 walioajiriwa na Leeds tangu walipofuzu kwa kipute cha EPL, walijaribu sana kuwarejesha katika Ligi Kuu mnamo 2005-06.

Ingawa walishushwa daraja hadi Ligi ya Daraja la Pili mnamo 2006 chini ya mkufunzi Simon Grayson, walirejea katika Championship mnamo 2010 chini ya kocha Jermaine Beckford.

Kuondoka kwa Beckford kulimpisha kocha Neil Warnock ambaye alihudumu kambini mwa Leeds kwa mwaka mmoja pekee kabla ya kumpisha Brian McDermott aliyempisha pia aliyekuwa mkufunzi wa Forest Green, David Hockaday.

Hockaday naye alitimuliwa baada ya kusimamia mechi sita pekee na nafasi yake ikatwaliwa na kocha Darko Milanic ambaye alikuwa mtangulizi wa Neil Redfearn, Uwe Rosler, Steve Evans, Garry Monk, Dane Thomas Christiansen na Paul Heckingbottom.

Ilikuwa hadi Juni 2018 ambapo Bielsa aliaminiwa na Andrea Radrizzani ambaye ni mmliki wa Leeds kudhibiti mikoba ya kikosi hicho. Hadi kuteuliwa kwake, alikuwa amenoa timu za taifa za Argentina na Chile na klabu ya Athletic Bilbao nchini Uhispania.

Hadi kufikia sasa, Bielsa amewaongoza Leeds kusajili ushindi katika jumla ya mechi 54 kutokana na 98 alizozisimamia.

Kati ya wanasoka ambao amewategemea pakubwa katika mafanikio ya kikosi chake msimu huu ni kiungo Kalvin Phillips, 24, na nahodha Liam Cooper.

You can share this post!

LISHE: Jinsi ya kutayarisha saladi ya parachichi (Guacamole)

COVID-19: Kenya yathibitisha visa 688 vipya ikiwa idadi ya...

adminleo