• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 8:22 PM
Lekuta na Manangoi kusaka ushindi Riadha za Diamond League

Lekuta na Manangoi kusaka ushindi Riadha za Diamond League

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA wapya wa Riadha za Dunia za Under-20, Solomon Lekuta na George Manangoi watatimka katika mbio za mita 1,000 kwenye Riadha za Diamond League mjini Monaco, Alhamisi usiku.

Lekuta alishinda ubingwa wa mbio za mita 800 naye Manangoi akabeba taji la mbio za mita 1,500 katika Riadha za Dunia za U20 zilizofanyika Julai 10-15 mjini Tampere nchini Finland.

Wawili hawa watapambania taji la mbio za mita 1,000 dhidi ya Wafaransa Mathieu Charles, Paul Chem-Lenhof, Anthony Crapanne, Baptiste Mischler na Thibault Larpin, Mbrazil Thiago Do Rosario Andre na Mswidi Andreas Kramer.

Wakenya Alfred Kipketer, Jonathan Kitilit na Cornelius Tuwei wako katika orodha ya wakimbiaji 12 watakaowania taji la mbio za mita 800. Ushindani mkali unatarajiwa kutoka kwa Mbotswana Nijel Amos, Mfaransa Pierre-Ambroise Bosse na raia wa Poland Marcin Lewandowski. Wakimbiaji kutoka Australia, Marekani, Canada na Uhispania pia watashiriki katika kitengo hiki.

Watimkaji saba kutoka Kenya watashiriki mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji za wanawake zilizovutia washiriki 16. Nyota Celliphine Chespol, ambaye alihifadhi taji la mbio hizi kwenye Riadha za Dunia za U20 mjini Tampere, anaongoza orodha ya Wakenya ambayo pia inajumuisha Beatrice Chepkoech, Roseline Chepng’etich, Daisy Jepkemei, Norah Jeruto, Caroline Tuigong na bingwa wa dunia mwaka 2015 Hyvin Kiyeng.

Bingwa wa Jumuiya ya Madola Aisha Praught na mzawa wa Kenya, Mbahraini Winfred Mutile ni baadhi ya wapinzani wakali Wakenya watakabiliana nao.

Kivumbi kikali kinatarajiwa katika mbio za mita 1,500 za wanaume ambazo zimevutia washiriki 16 akiwemo bingwa wa Jumuiya ya Madola Elijah Manangoi na Timothy Cheruiyot ambaye amekuwa akitetemesha sana mwaka huu.

Mbali na Manangoi na Cheruiyot, Wakenya wengine ambao wako mjini Monaco kutafuta fahari katika kitengo hiki ni Jackson Kivuva, Ferguson Rotich na Charles Simotwo. Watakabiliana na washiriki kutoka Marekani, Norway, Uingereza, Djibouti, Ethiopia, Uholanzi, Morocco na Jamhuri ya Czech.

Mbio za mita 3,000 kuruka maji na viunzi za wanaume zinatarajiwa kuwa moto hasa baada ya kuvutia majina makubwa kama bingwa dunia, Olimpiki na Jumuiya ya Madola Conseslus Kipruto kutoka Kenya pamoja na Muamerika Evan Jager.

Wakenya wengine hapa ni Nicholas Kiptanui Bett, Abraham Kibiwot, Emmanuel Kiprono na Kenndy Njiru. Kuna washiriki wengine kutoka Marekani, Ethiopia, Morocco, Canada na Uswidi katika kitengo hiki kitakachofunga mashindano haya ya siku moja.

You can share this post!

Harambee starlets watiwa adabu na Crested Cranes

Ulinzi yapanga kuinyeshea Vihiga mvua ya magoli

adminleo