Michezo

Lemngole alivyong’aa kwenye mvua Diamond League, Wanyonyi alowa maji bure

Na GEOFFREY ANENE August 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

DORIS Lemngole kutoka Chuo Kikuu cha Alabama nchini Amerika alionja ushindi wake wa kwanza kabisa katika mashindano ya riadha za Diamond League baada ya kuponyoka na taji la mita 3,000 kuruka viunzi na maji duru ya Lausanne nchini Uswisi, Jumatano usiku.

Lemngole, ambaye hakumaliza 3,000m kuruka viunzi na maji mara ya kwanza alishiriki Diamond League wakati wa duru ya Doha nchini Qatar mwezi Mei 2023, alinyakua taji la Lausanne kwa dakika 9:16.36 na tuzo ya Sh1.2 milioni.

Lemngole guu kwa lingine kitengo chake cha 3,000m kuruka viunzi na maji katika uwanja wa Stade olympique de la Pontaise mjini Lausanne. PICHA | REUTERS

Kutoka orodha ya washiriki 12, Lemngole alifuatwa kwa karibu na Muethiopia Sembo Almayew (9:20.39) na Mwamerika Olivia Markezich (9:20.73) waliovuna Sh775,200 na Sh 516,800, mtawalia.

“Kukimbia kwenye mvua haikuwa rahisi. Hata hivyo, nisalia makini na pia nikajituma na kupata ushindi huu. Sikupata muda niliokuwa natafuta, lakini changmoto kama hizi zinaniandaa vyema kwa msimu uliosalia na Riadha za Dunia,” alisema Lemngole, 23.

Mambo hayakuwa mazuri kwa bingwa wa Olimpiki wa 800m, Emmanuel Wanyonyi, aliyeduwazwa na Muingereza Josh Hoey katika mbio hizo za kuzunguka uwanja mara mbili.

Emmanuel Wanyonyi akishiriki 800m riadha za Diamond League duru ya Monaco awali Julai 2025. Alionjeshwa kivumbi duru ya Lausanne nchini Uswisi siku ya Jumatano. PICHA | REUTERS

Wanyonyi alitia mfukoni Sh775,200 baada ya kuandikisha muda wa 1:43.29. Ni muda wake mbovu kutoka mashindano matano yaliyopita.

Hoey alitwaa ubingwa kwa 1:42.82 naye Mhispania Mohamed Attaoui akafunga tatu-bora (1:43.38). Mshindi wa dunia Marco Arop kutoka Canada alikamata nafasi ya tano kutoka orodha ya watimkaji 10 kwa 1:43.91.

Mzawa wa Kenya, Isaac Kimeli anayekimbilia Ubelgiji, alitawala 5,000m kwa 13:07.67 akifuatiwa na Mwamerika Grant Fisher (13:08.51) na Eduardo Herrera kutoka Mexico (13:09.50).

Wakenya Ishmael Kipkurui (13:09.82), Edwin Kurgat (13:09.91), Denis Kipkoech (13:13.97) na Jacob Krop (13:18.65) hawakuwa na lao wakimaliza nambari tano, sita, 10 na 14 kutoka orodha ya washiriki 21, mtawalia.

Ligi hiyo duru 15 itakamilika na fainali mjini Zurich, Uswisi hapo Agosti 27-28.