Leo macho yote kwa Mourinho wakati Spurs inakwaana na West Ham
Na MASHIRIKA
LONDON, Uingereza
ULIMWENGU wa soka unasubiri kwa hamu kubwa kuona jinsi Jose Mourinho atakavyoanza maisha kama kocha wa Tottenham Hotspur itakayozuru West Ham kwa mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza(EPL) hii leo Jumamosi.
Kocha huyo wa zamani wa Manchester United na Chelsea ametwikwa majukumu ya kuokoa kampeni ya Spurs, iliyompiga kalamu Mauricio Pochettino siku chache zilizopita.
Raia huyo Mreno anafaa kutatua masuala kadhaa, ikiwemo kupata suluhisho kwa rekodi mbaya ya ugenini ya Spurs, ambayo haina ushindi ligini tangu Januari.
Spurs, ambayo ilifika fainali ya Klabu Bingwa Ulaya msimu uliopita, imekuwa na matokeo ya kusikitisha mwaka huu.
Inashikilia nafasi ya 14 baada ya kupata ushindi katika mechi tatu pekee kati ya 12 zilizopita.
Hata hivyo, itaanza mchuano huu na motisha ya kuwa imeilemea West Ham kwenye mechi tatu zilizopita za ugenini.
Nambari 16 West Ham pia imepoteza mwelekeo tangu ipige Manchester United mnamo Septemba 22.
Harry Kane, Dele Alli na Son Heung-min ni baadhi ya wachezaji ambao Mourinho atatumai watamuanzishia maisha vyema Spurs.
Kiungo Victor Wanyama, ambaye ni nahodha wa timu ya taifa ya Kenya, alitumiwa kwa uchache na Pochettino msimu huu.
Baada ya Mourinho kuwasili Tottenham, baadhi ya Wakenya wanaamini kuwa atafufua mchezo wa Wanyama, ambaye hata hivyo hatarajiwi kuanzishwa leo.
West Ham itawategemea Robert Snodgrass na Michail Antonio, aliyezamisha Spurs zilipokutana mara ya mwisho mwezi Aprili.