• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Leopards kusubiri Sharks gozi la Ligi

Leopards kusubiri Sharks gozi la Ligi

Na JOHN ASHIHUNDU

MECHI za Ligi Kuu ya Kenya (KPL) zitarejelewa wikendi hii baada ya likizo ya wiki mbili.

Baada ya kuanza msimu vibaya kufuatia kichapo cha 1-0 mikononi mwa Kakamega Homeboyz, AFC Leopards itakuwa MISC, Kasarani kualika Kariobangi Sharks kuanzia saa tisa.

Kikosi hicho kitaongozwa na naibu nahodha Wyvonne Isuza anayeshikilia usukani baada ya Robinson Kamura kupatwa na jeraha.

Timu hizo zilifungana 1-1 msimu uliopita, lakini huenda Ingwe wakafanikiwa kupata ushindi baada ya kufanya usajili wa nguvu majuzi.

Mabingwa hao wa KPL mara 13 wamesajili wanasoka matata akiwemo mshambuliaji hodari John Mark Makwatta ambaye aliwahi kuchezea Ulinzi Stars.

Mbali na mshambuliaji huyo wa kimataifa, kadhalika Ingwe walifanikiwa kuwanasa Kevin Kimani kutoka Mathare United, Clyde Senaji kutoka Tusker FC pamoja na beki wa upande wa kushoto Washington Munene kutoka Wazito FC.

Nyota wengine waliojiunga na Leopards ni beki Robert Ayala Mudenyi kutoka Sony Sugar, Soter Kayumba kutoka Sofapaka na Collins Shivachi aliyekuwa na Tusker.

Leopards pia imeimarisha safu yao ya ushambuliaji kwa kumrejesha Paul Were anayetarajiwa kushirikiana vyema na Ismail Diarra ambaye aliwahi kuchezea Azam, Al Ismaily na DC Derling Motema Pembe ya DR Congo pamoja na Vincent Abamahoro kutoka Kiyyuvu Sports ya Rwanda.

Kadhalika, Ingwe imefanikiwa kumpata kiungo wa kimataifa Tresor Ndikumana ambaye atashirikiana na Isuza pamoja na kipa Benjamn Ochan kutoka Uganda ambaye amejaza nafasi ya Eric Ndayisimiye.

Ubingwa wa bara

Lakini kutokana na ratiba ya mechi za mchujo kuwania ubingwa wa bara, Gor Mahia na Bandari hazitashiriki katika michuano hiyo.

Gor Mahia watakuwa ugenini kucheza na USM Alger ya Algeria Jumapili katika pambano la mchujo la Klabu Bingwa barani Afrika na sasa wamepangiwa kuregea ligini katikati mwa wiki.

Mechi hiyo itachezewa Mustapha Tchaker Stadium, wakati Bandari wakipeperusha bendera ya taifa pia kesho ugani Kasarani katika mechi za Confederations Cup dhidi ya US Ben

Gor walitarajiwa kucheza na Chemelil mjini Kisumu, lakini sasa mechi hiyo imehamishwa hadi Alhamisi. Bandari walitarajiwa kualika Zoo kwao Mombasa.

You can share this post!

KITANUKA: Liverpool yaalika Newcastle

UMBEA: Changamoto za kunyoosha viungo na mwenzako kazini

adminleo