Lewandowski acheka na nyavu mara tatu na kuvunja rekodi ya ufungaji wa mabao katika soka ya Ujerumani
Na MASHIRIKA
FOWADI Robert Lewandowski aliendelea kuweka historia zaidi kwenye ulingo wa soka kwa kufunga mabao matatu kwenye ushindi wa 5-0 dhidi ya Eintracht Frankfurt.
Lewandowski ambaye ni raia wa Poland ndiye mwanasoka wa kwanza kuwahi kufunga mabao 10 ya Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) katika mechi tano za ufunguzi wa msimu.
Licha ya ushindi huo mnono uliosajiliwa na Bayern, pigo kubwa kwa miamba hao wa bara Ulaya ni jeraha la mguu ambalo huenda likamweka nje beki wa kushoto Alphonso Davies kwa kipindi kirefu.
Nyota huyo raia wa Canada aliumia katika dakika ya pili ya mechi na huenda akakosa kucheza tena katika mechi nyingine yoyote ya msimu huu wa 2020-21.
Lewandowski aliwafungulia Bayern ukurasa wa mabao katika dakika ya 10 kabla ya kupachika wavuni goli la pili katika dakika ya 26 baada ya kushirikiana vilivyo na sajili mpya Douglas Costa.
Leroy Sane na Jamal Musiala walikuwa wafungaji wa mabao mengine ya Bayern ambao waliweka historia ya kucheka na nyavu mara 22 kutokana na mechi tano za kwanza za msimu wa Bundesliga.
Mwingereza Musiala, 17, ndiye mchezaji was aba wa Bundesliga kuwahi kufunga zaidi ya bao moja la Bundesliga kabla ya kufikisha umri wa miaka 18.
Ushindi wa Bayern ambao kwa sasa wanatiwa makali na kocha Hansi Flick uliwapaisha hadi kileleni mwa jedwali la Bundesliga kwa alama 12 kutokana na mechi tano. Ni pengo la pointi moja pekee ndilo linalotamalaki kati ya Bayern na RB Leipzig waliopaa hadi nafasi ya pili baada ya kuwacharaza Hertha Berlin 2-1.
Katika msimu uliopita wa 2019-20, Lewandowski, 32, alifunga mabao tisa kutokana na mechi tisa za ufunguzi wa msimu na kufikia rekodi iliyowekwa na aliyekuwa mwanasoka wa Borussia Monchengladbach, Peter Meyer mnamo 1967-68.
Mnamo 2019-20, Lewandowski alicheka na nyavu za wapinzani mara 55 kutokana na mechi 47 kwenye mashindano yote; na akafunga magoli 34 katika mechi 31 za Bundesliga.
Ilivyo, rekodi yake ya msimu huu ni wastani wa bao moja kila baada ya dakika 37 ligini.
Kati ya mabao yake yote ya hadi sasa msimu huu, 10 yametokana akipangwa kwenye kikosi cha kwanza. Mchuano wa pekee alioukamilisha bila bao ni ule uliomshuhudia akiingia ugani katika kipindi cha pili na chombo cha waajiri wake kuzamishwa kwa kichapo cha 4-1 na Hoffenheim mnamo Septemba 2020.