Liverpool hawana haja na Messi – Klopp
Na CHRIS ADUNGO
KOCHA Jurgen Klopp amefutilia mbali uwezekano wa fowadi mahiri wa Barcelona, Lionel Messi kujiunga na kikosi chake cha Liverpool nchini Uingereza.
Hata hivyo, mkufunzi huyo mzawa wa Ujerumani amekiri kwamba ujio wa Messi katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kutainua zaidi viwango vya ubora na ushindani katika kivumbi hicho.
Mustakabali wa Messi kambini mwa Barcelona bado haujulikani tangu mshambuliaji huyo mzawa wa Argentina awasilishe barua kwa waajiri wake akiwataka wamwachilie atafute hifadhi kwingineko.
“Sioni uwezekano wowote wa Messi kuwa sehemu ya kikosi cha Liverpool muhula huu,” akatanguliza Klopp.
Alipoulizwa iwapo angependa kumsajili Messi mwenye umri wa miaka 33, Klopp alisema: “Ni kocha yupi asiyetaka kujivunia huduma za Messi katika kikosi chake?”
“Tayari tuna idadi ya kutosha ya wanasoka. Hivyo, hatuwezi kumsajili. Pili, bei yake inatisha. Hivyo, hatuwezi kumudu gharama yake kwa sasa. Lakini kusema kweli, ni mchezaji wa haiba kubwa ambaye atafanya EPL kuwa kivutio kikubwa iwapo atahiari kutua katika soka ya Uingereza,” akasema Klopp.
Messi amehusishwa na uwezekano mkubwa wa kuungana na aliyewahi kuwa kocha wake kambini mwa Barcelona, Pep Guardiola ambaye kwa sasa anawatia makali vijana wa Manchester City.
“Kuja kwa Messi kambini mwa Man-City kutawafanya wapinzani hao wetu kuwa vigumu kupigika,” akasema Klopp.
Man-City ambao walikuwa washindani wakuu wa Liverpool katika EPL msimu uliopita, bado hawajasema lolote kuhusiana na tetesi zinazowahusisha na Messi.
Hata hivyo, wamefutilia mbali uwezekano wa nyota Bernardo Silva, Riyad Mahrez na Gabriel Jesus kujiunga na Barcelona katika juhudi za miamba hao wa soka ya Uingereza kumsajili Messi.
“Kwa minajili ya kufanya EPL kuwa kivutio, itakuwa vyema kwa Messi kuja Uingereza. Hata hivyo, sina uhakika iwapo EPL itahitaji kupigwa jeki kiasi hicho,” akaendelea Klopp.
“Messi hajawahi kucheza soka katika ligi yoyote nje ya La Liga. Soka katika kila taifa ni tofauti. Ningependa sana kuona jinsi EPL itakavyokuwa na Messi japo sina uhakika iwapo hilo litatimia,” akaongeza Klopp.
Liverpool wanaendelea kujifua kwa minajili ya msimu ujao wa 2020-21. Kabla ya kufungua rasmi msimu wao wa EPL, Liverpool wamepangiwa kuvaana na Arsenal ambao ni washindi wa Kombe la FA kwenye gozi la Community Shield mnamo Jumamosi ya Agosti 29.
Licha ya kusisitiza kwamba anaridhishwa na ukubwa wa kikosi chake kwa sasa, Klopp amedokeza uwezekano wa kuendelea kusajili wanasoka wapya watakaoimarisha zaidi idara muhimu kambini mwa Liverpool kufikia Oktoba 5, 2020, ambayo ni siku ya mwisho ua uhamisho wa wachezaji.
“Tuna idadi ya kutosha ya wanasoka. Muhimu zaidi ni kwamba tuna mseto mzuri wa chipukizi na masogora wazoefu wa haiba kubwa. Fursa ikijipa na fedha zikipatikana, hatutasita kusajili wachezaji wachache zaidi kwa minajili ya kuboresha kikosi hata zaidi,” akaongeza kocha huyo wa zamani wa Borussia Dortmund ya Ujerumani.