Michezo

Liverpool kunyanyua kombe la EPL nyumbani Anfield

July 22nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

LIVERPOOL watapokezwa kombe la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) waliloshinda msimu huu mwishoni mwa mechi itakayowakutanisha leo usiku Jumatano ya Julai 22, 2020 na Chelsea uwanjani Anfield.

Kocha Jurgen Klopp amesema kunyanyua taji hilo kutakuwa sawa na “Krismasi” kwake.

“Imekuwa safari ndefu kabla ya kufikia hapa tulipo. Tumekuwa mabingwa wa EPL kwa mwezi mmoja uliopita, na hatimaye tutatawazwa wafalme rasmi hii leo,” akatanguliza Klopp.

“Ni kama Krismasi ambapo unajua unapata zawadi fulani mahsusi kisha ulazimike kusubiri tena kwa kipindi kirefu ndipo zawadi nyingine kwa minajili ya kusherehekea kitu hicho hicho ije,” akasema mkufunzi huyo mzawa wa Ujerumani.

Klopp ambaye aliwaongoza Liverpool kutia kapuni ubingwa wa taji la EPL kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30 aliongeza: “Itakuwa spesheli. Nafurahi sana vijana wangu hatimaye watakuwa na kipindi hicho cha kusherehekea ushindi wao. Wanastahili zaidi kuliko yeyote mwingine kwa sababu tunaelewa matukio mengi ambayo wamekabiliana nayo hadi kufikia leo.”

Ingawa hivyo, Klopp amewataka masogora wake kumakinikia zaidi mchuano wao ambao utakuwa wa pili kutoka mwisho wa kampeni za msimu huu badala ya kuweka mawazo zaidi kwenye kombe.

“Ladha ya kunyanyua kombe hili itakolezwa zaidi na ushindi dhidi ya Chelsea. Hii ni mechi ambayo imekuwa vigumu zaidi kwangu kujiandaa kwayo kwa sababu yapo mambo mawili yatakayofanyika leo usiku: kucheza dhidi ya kikosi kilicho na maazimio makubwa ligini na kusherehekea ufalme,” akasema Klopp, 53.

Japo anauguza jeraha, nahodha Jordan Henderson atawaongoza wenzake wa Liverpool kunyanyua taji la EPL katika jukwaa maalum ambalo tayari limejengwa katika uwanja wa Anfield.

Mkuu wa Polisi katika jiji la Merseyside, Andy Cooke amewaonya mashabiki wa Liverpool dhidi ya kukongamana nje ya uwanja wa Anfield kusherehekea tukio la Liverpool kunyanyua ubingwa wa soka ya Uingereza kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30 ya kusubiri.

Klopp amesema kwamba gwaride la heshima litakaloshirikisha maelfu ya mashabiki litaandaliwa kwenye barabara kuu za Merseyside baada ya janga la corona kudhibitiwa vilivyo.